• HABARI MPYA

    Friday, April 27, 2018

    KOCHA MPYA MKONGO WA YANGA SC ATOA MBINU MPYA ZA ‘KUUA MNYAMA’ JUMAPILI TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA mpya wa Yanga SC, Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) amewapa mbinu mpya wachezaji wa timu hiyo kuelekea mchezo na mahasimu wa jadi, Simba SC Jumapili.
    Yanga SC watakuwa wageni wa Simba SC Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mchezo huu unakuja wiki tatu tangu klabu hiyo ikimbiwe na aliyekuwa kocha wake, Mzambia George Lwandamina ambaye amerejea kwao ikielezwa anataka kujiunga tena na Zesco United ya huko.
    Na baada ya waliokuwa wasaidizi wa Lwandamina kuiongoza timu katika mechi tatu bila ushindi, ikitoa sare mbili zote za Ligi Kuu na zote 1-1 dhidi ya Singida United na Mbeya City katikati ya kipigo cha 1-0 cha Wolaita Dicha mjini Hawassa Ethiopia katika Kombe la Shirikisho, uongozi umeleta kocha mpya.
    Huyo ndiye Zahera ambaye baada ya kufika kambini Morogoro alianza kwa kukutana na makocha waliopo, Mzambia Noel Mwandila na wazawa Nsajigwa Shadrack na kocha wa makipa, Juma Pondamali.
    Habari kutoka kwenye kambi ya Yanga mjini Morogoro zimesema kwamba Zahera amepata fursa ya kuitazama Yanga SC inavyocheza katika mechi zake kadhaa zilizopita na kuwatazama pia Simba SC kabla ya kuingia mazoezini kutoa mbinu zake kusaidia maandalizi ya pambano dhidi ya watani Jumapili.
    Zahera hatakaa benchi Jumapili na kimsingi ataanza kazi rasmi kwenye mechi za makundi Kombe la Shirikisho, Yanga ikianzia ugenini dhidi ya USMA Alger Mei 7, mwaka huu mjini Algiers.
    Simba SC iliyo chini ya kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia, Aymen Mohamed Hbibi, Mrundi, Masoud Juma na mzawa Muharami Mohamed ‘Shilton’ inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 59 baada ya kucheza mechi 25, wakati Yanga inafuatia kwa mbali kidogo ikiwa na pointi zake 48 za mechi 23.
    Yanga inazidiwa pointi 11 na Simba SC na ina viporo viwili, maana yake ili kutetea ubingwa wao, itabidi washinde Jumapili na washinde mechi zao zote zilizobaki za Ligi Kuu, huku wakiwaombea mahasimu wao hao wapoteze mechi nyingine pia moja – jambo ambalo hakika ni gumu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA MPYA MKONGO WA YANGA SC ATOA MBINU MPYA ZA ‘KUUA MNYAMA’ JUMAPILI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top