• HABARI MPYA

    Monday, April 23, 2018

    YANGA SC WAKATA RUFAA MECHI NA MBEYA CITY…MKWASA ASEMA WACHEZAJI WAKE WALICHEZA KWA HOFU BAADA YA KUANZA KUSHAMBULIWA KWA MAWE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa klabu ya Yanga umewasilisha rufaa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya mchezo wa jana wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya ikilalamikia wapinzani wao kuchezesha wachezaji zaidi na pia vurugu zilizojitokeza.
    Katibu Mkuu wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba hakukuwa na sababu yoyote mchezo wa jana kuendelea baada ya dakika ya 69 kutokana na vurugu kubwa zilizojitokeza uwanjani, mashabiki wa Mbeya City wakirusha mawe na silaha nyingine.
    “Wachezaji wangu walipatwa na wasiwasi na kupunguza kwa kiasi kikubwa fikra za kimchezo na zaidi wakicheza kwa hofu ya kuogopa kupigwa mawe, jambo ambalo liliwaruhusu wenyeji kuuteka mchezo hadi kupata bao la kusawazisha,”amesema Mkwasa.
    Katibu Mkuu wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa (kulia) amesema hakukuwa na sababu yoyote mchezo wa jana dhidi ya Mbeya City kuendelea baada ya dakika ya 69  

    “Kipa wetu, (Youthe Rostand) mara mbili aliliacha lango wazi na kwenda katikati kabisa ya Uwanja kunusuru maisha yake baada ya kuanza kushambuliwa kwa mawe na mashabiki wa Mbeya City, jambo ambalo refa na wasaidizi wake wote, hata Kamisaa waliona. Ni kwa sababu hizo tumekata rufaa,”amesema Mkwasa.  
    Lakini pia, Mkwasa amesema kwamba katika rufaa yao wamelalamikia pia wapinzani wao kuchezesha wachezaji zaidi uwanjani. 
    Matumaini ya Yanga SC kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara yalizidi kufifia jana baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Mbeya City Uwanja wa Sokoine.
    Matokeo hayo yanaiongezea Yanga SC pointi nyingine moja, wakifikisha 48 katika mechi 23, wakizidiwa pointi 11 na vinara, Simba SC wenye pointi 59 za mechi 25 na wababe hao watakutana Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa, Shomari Lawi wa Kigoma aliyesaidiwa na Omari Juma wa Dodoma na Godfrey Kihwili wa Arusha, Yanga ilitangulia kupata bao lake kipindi chake cha kwanza, kupitia kwa Raphael Daudi Loth kabla ya MCC kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Iddi Suleiman Nado.
    Frank Ikobela wa Mbeya City akimiliki mpira mbele ya wachezaji wa Yanga jana Uwanja wa Sokoine 

    Mbeya City walianza kulitia misukosuko lango la Yanga dakika ya nne tu, baada ya mshambuliaji wake tegemeo, Frank Ikobela kupiga shuti lililozuiwa na beki Juma Abdul na kuwa kona ambayo iliokolewa. Yanga SC ilijibu shambulizi hilo dakika ya 14 baada kiungo Pius Buswita kutia krosi nzuri iliyopanguliwa na kipa Owen Chaima na mpira kumkuta kiungo Raphael Daudi ambaye alipojaribu kuurudisha ukaokolewa na kipa huyo Mmalawi.
    Chaima akafanya kazi nzuri tena dakika ya 16 kwa kuokoa mpira uliopigwa na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyepokea pasi nzuri ya kiungo mzawa, Yussuf Mhilu
    Mbeya City wakazinduka dakika ya 20 baada ya mshambuliaji wao, Eliud Ambokile kupiga mpira wa juu kiufundi kufuatia pasi ya kiungo Mohammed Samatta ukagonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya beki wa kushoto, Gardiel Michael kuondosha kwenye hatari.
    Kipa wa Yanga, Mcameroon Youthe Rostand akafanya kazi nzuri ya kudaka mpira uliogongwa kwa kifua na Victor Hangaya dakika ya 34 kufuatia krosi ya mwasapili ambapo kipa anadaka.
    Kaimu Nahodha wa Yanga SC, Kevin Patrick Yondan alishindwa kuendelea na mchezo baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, nafasi yake ikichukuliwa na Nahodha Mkuu, mkongwe Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
    Yanga ikaanza kufunguka zaidi kipindi cha pili kwa kupeleka mashambulizi ya moja kwa moja hususan baada ya mabadiliko mengine yaliyofanywa akitolewa kiungo Emmanuel Martin na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mahadhi.
    Hiyo iliiwasaidia wana Jangwani hao kupata bao dakika ya 58, kiungo Raphael Daudi Loth akiiadhibu timu yake ya zamani kwa shuti kali baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu na beki wa kulia, Juma Abdul kufuatia Mahadhi kuangushwa.
    Baada ya bao hilo, mashabiki wa Mbeya City wakaanza kufanya fujo wakitupa mawe uwanjani na moja likamgonga kiichwani kipa wa Yanga, Youthe Rostand.
    Mchezo ukaendelea baada ya dakika mbili, lakini dakika ya 65 beki wa Mbeya City Ramadhani Malima akatolewa kwa kadi nyekundu, baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kumfuatia kumchezea rafu kiungo wa Yanga, Yussuf Mhilu.
    Vurugu zikaibuka tena Uwanja wa Sokoine masabiki wakipiga mawe na Polisi wakalazimika kutumia gesi za machozi kutuliza vurugu, kabla ya mchezo huo kuendelea tena dakika tano baadaye kufuatia ulinzi kuimarishwa kwa gari lingine la aksari wa kupambana na Ghasia kuingia uwanjani.
    Mchezo wa kujihami kulinda bao dakika za mwishoni uliwagharimu Yanga kuwapa wenyeji bao la kusawazisha, lililofungwa na Iddi Suleiman Nado dakika ya 90 kwa kichwa akimalizia krosi ya Kenny Kunambi.
    Bao hilo liliwachanganya Yanga na kuwaruhusu Mbeya City kutawala mchezo zaidi kuelekea filimbi ya mwisho.  Mbeya City walifanya mabadiliko dakika ya saba ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 kwa kumuingiza Danny Joram wakati Eliud Ambokile ametolewa nje kutibiwa.
    Lakini Ambokile alipomaliza kupewa matibabu akarejea uwanjani na kufanya Mbeya City wawe na jumla ya wachezaji 11 uwanjani, licha ya mmoja, Malima kutolewa kwa kadi nyekundu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAKATA RUFAA MECHI NA MBEYA CITY…MKWASA ASEMA WACHEZAJI WAKE WALICHEZA KWA HOFU BAADA YA KUANZA KUSHAMBULIWA KWA MAWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top