• HABARI MPYA

    Friday, April 27, 2018

    BUNGE LAAGIZA UCHUNGUZI HARUFU UFISADI MAPATO UWANJA WA TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DODOMA
    BUNGE limeiagiza serikali kufanya uchunguzi wa 'Fedha za Mchina' zinazokatwa katika mapato ya kila mechi inayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Pia limeitaka serikali kuhakikisha kuwakuwa na udhibiti wa mapato ya mechi za soka kwa kuuza tiketi kwa mfumo wa kieletroniki kwa kuwa fedha nyingi zimekuwa zikiibwa.
    Akiwasilisha bungeni mjini hapa leo maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka ujao wa fedha, mjumbe wa kamati hiyo, Deogratius Ngalawa, amesema kamati inatambua mapato ya Uwanja wa Taifa na Uhuru ni makubwa lakini nchi inakabiliwa na tatizo la udanganyifu katika taarifa za mapato hayo.


    "Kumekuwa na fedha zinazojulikana kwa jina la fedha za Mchina kwa kila mchezo kwa kuwa wamekuwa wakilipwa Wachina wanaohudumia uwanja," amesema Ngalawa.
    Mbunge huyo wa Ludewa (CCM) ameongeza: "Kamati imehoji kuhusu suala hili lakini haijapata maelezo ya kuridhisha, hivyo inashauri uchunguzi ufanywe kuhusu fedha za Mchina zinazokatwa katika kila mchezo na Bunge lako tukufu lipewe taarifa."
    Amesema kamati yao pia inashauri mapato ya Uwanja wa Taifa na Uhuru yasichanganywe kwa kuwa wamebaini yamekuwa yakichanganywa kwa makusudi ili kuwachanganya wadau.
    Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu udanganyifu wa mapato ya mechi za soka nchini huku serikali ikichukua hatua mbalimbali bila mafanikio ya kutosha.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BUNGE LAAGIZA UCHUNGUZI HARUFU UFISADI MAPATO UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top