• HABARI MPYA

    Sunday, April 01, 2018

    MWANTIKA AHAMISHIWA MUHIMBILI BAADA YA KUUMIA JANA CHAMAZI

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    BEKI wa Azam FC, David Mwantika, anaendelea vizuri baada ya kupata hitilafu ya mwili wakati wa mchezo wa wa Robo Fainali ya Azam Sporst Federation Cup (ASFC) dhidi ya Mtibwa Sugar usiku wa kuamkia leo.
    Mwantika alipata tatizo hilo dakika ya 64 na kupatiwa matibabu ya awali kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Mbagala Zakhem na kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke, na baadaye ile ya Rufaa ya Muhimbili (MNH).
    Daktari wa Azam FC, Dk. Mwanandi Mwankemwa, anayeshughulikia taratibu za matibabu yake ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba beki huyo anaendelea vizuri na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.
    Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' akiwa pembeni ya David Mwantika hospitalini
    “Alikuwa kwenye hali mbaya mara baada ya kumkimbiza hospitali, alikuwa amezimia lakini tunashukuru Mungu kwa sasa anaendelea vizuri, alipata matibabu ya awali Mbagala Zakhem kabla ya kuomba ahamishiwe Muhimbili baada ya kwenda Hospitali ya ya Wilaya ya Temeke zoezi lililokamilika saa saba usiku.
    “Tunamshukuru Mungu majira ya saa 10 alfajiri alizinduka na kuanza kuwatambua watu na kuongea, na asubuhi ya leo amekunywa chai vizuri na kuendelea na matibabu huku akiwa yupo kwenye hatua za kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupata nafuu,” alisema.
    Aidha taratibu zinazofanyika hivi sasa kabla ya kuruhusiwa, ni beki huyo kufanyiwa uchunguzi wa moyo ili kufahamu kuwa kama ana tatizo hilo.
    “Mara baada ya kujisikia vizuri kabla ya kuruhusiwa kuondoka hivi sasa amehamishiwa kwenye wodi ya Taasisi ya Jakaya Kikwete inayojihusisha na matatizo ya moyo, ambapo atafanyiwa uchunguzi wa moyo ili kujua kama ana tatizo hilo na baadaye watatoa majibu ya vipimo na ushauri mwingine kwa wanavyomuona,” alimalizia Dk. Mwankemwa.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWANTIKA AHAMISHIWA MUHIMBILI BAADA YA KUUMIA JANA CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top