• HABARI MPYA

  Tuesday, April 10, 2018

  YANGA KUITUMIA MECHI NA SINGIDA UNITED KESHO KAMA SEHEMU YA MAANDALIZI YA MCHEZO WA MARUDIANO NA WOLAITA DITCHA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mzambia wa Yanga, George Lwandamina amesema kwamba atautumia mchezo dhidi ya Singida United kesho kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wa marudiano na Wolaita Ditcha wiki ijayo nchini Ethiopia.
  Yanga SC inatarajiwa kuwakaribisha Singida United kesho Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikihitaji ushindi ili kuweka hai matumaini ya kutetea taji lao.
  Yanga itaingia kwenye mchezo wa kesho ikitoka kushinda 2-0 dhidi ya Wolaita Ditcha ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi Uwanja wa Taifa.

  George Lwandamina amesema mchezo dhidi ya Singida utakuwa mgumu kesho

  Na timu hizo zinatarajiwa kurudiana Jumatano ya wiki ijayo, Aprili 18 Uwanja wa Hawassa mjini Hawassa nchini Ethiopia kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Lwandamina amesema kwamba mchezo dhidi ya Singida utakuwa mgumu, lakini watajitahidi washinde ili kujiweka kwenye nafasi nzuri.
  “Singida ni timu nzuri na tumetoka kucheza nayo wiki iliyopita tu pale Singida kila mtu ameona matokeo, maana yake mechi ya Jumatano itakuwa ngumu, vizuri hata wachezaji wangu wanalijua hilo. Tunajipanga. Kwetu tutautumia mchezo huu pia kama sehemu ya maandalizi yetu ya mechi ya marudiano na Ditcha,”amesema Lwandamina.
  Mapema mwezi huu, Aprili 1 Singida United waliitupa nje Yanga SC kwenye Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup kwa ushindi wa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Namfua mjini Singida.
  Hivyo kesho Yanga pamoja na kuhitaji pointi kwa ajili ya kuongeza kasi ya kuwafukuzia mahasimu wao, Simba SC pale kileleni, lakini pia itataka kulipa kisasi kwa timu ya kocha wao wa zamani, Mholanzi, Hans van der Pluijm. 
  Kwa ujumla, Ligi Kuu inaendelea leo kwa mchezo mmoja tu, Mwadui FC wakiwakaribisha Lipuli FC Uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga, wakati mechi nyingine ya kesho itakuwa ni kati ya Tanzania Prisons na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mbao FC na Njombe Mji FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Hiyo ni baada ya Simba SC jana kuwachapa wenyeji, Mtibwa Sugar 1-0 bao pekee la mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Ushindi unaifanya Simba SC ifikishe pointi 52 baada ya kucheza mechi 22 na kuendeleza kuongoza Ligi Kuu kwa pointi sita zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 46 za mechi 21.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KUITUMIA MECHI NA SINGIDA UNITED KESHO KAMA SEHEMU YA MAANDALIZI YA MCHEZO WA MARUDIANO NA WOLAITA DITCHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top