• HABARI MPYA

    Tuesday, August 08, 2017

    TARAJIA HAYA KATIKA SOKA YA TANZANIA SHIJA RICHARD AKIWA RAIS WA TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MGOMBEA Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Shija Richard Shija katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Jumamosi ya Agosti 12 mkoani Dodoma ameahidi kuleta mapinduzi makubwa katika mchezo huo nchini.
    Katika Mkutano wake na Waandishi wa Habari leo, Shija amesema kwamba soka ya Tanzania inahitaji ufufuo naye ndiye chaguo sahihi atakayeweza kurejesha uhai wa mchezo huo nchini. 
    Ifuatayo ni taarifa kamili ya Shijja Richard juu ya mkakati wake wa kuinua soka ya Tanzania “Uhalisia ni kuwa kwa wale watakaochaguliwa watakuwa na fursa ya kuongoza kwa
    miaka minne. Siku hizi hakuna biashara ya mapinduzi kwenye mpira wa miguu.
    Ni dhahiri kuwa kila aliyeingia kwenye uchaguzi ana ajenda hata kama anagombea
    nafasi ya ujumbe. Ajenda inabebwa na malengo ya mgombea kama alivyoyaanisha au
    kuyataja katika fomu yake ya kuomba uteuzi.
    Hivyo wagombea wana wajibu wa kutangaza ajenda zao mbele ya wapiga kura ambao
    ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.
    Mpira wa miguu ndani ya uwanja na nje ya uwanja (uongozi) umetoka wapi na sasa uko wapi. Ikiwa kila mgombea amelifanyia utafiti hilo, basi atakuwa na ajenda
    iliyomsukuma na yeye kuingia kuchangia ustawi na maendeleo ya mpira wa miguu nchini katika ngazi hiyo ya juu.
    Shijja Richard akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam

    Ajenda ya mgombea haiwezi kunakshiwa kwa kusema fulani hakuwa kiongozi mzuri, fulani hana uzoefu wala fulani hivi, bali itatiwa nakshi na maelezo ya kwa nini huu
    ndiyo wakati wake na njia zipi zitatumika kuitekeleza.
    Katika uongozi wangu nitaweka Dira (Vision) ili kila mwanafamilia ya mpira aweze
    kutambua uelekeo wetu kama taasisi. Pia Dira hiyo itaenda sambamba na dhima
    (Mission).
    Naamini kampeni za matusi, kashfa, kejeli hazina nafasi katika uchaguzi wa TFF
    ambayo ni taasisi inayoheshimika- kubwa ikiwa inasimamia mchezo ambao si tu
    unaongozwa kwa kupendwa Tanzania bali duniani kote kwa ujumla.
    KAMPENI ZA UCHAGUZI NAFASI YA RAIS WA TFF
    Kampeni zangu zitajikita zaidi kutangaza sera na mikakati niliyonayo nitakapopewa
    fursa ya kuiongoza TFF.
    Rais wa TFF ni nafasi kubwa, ndiye kiongozi Mkuu wa shirikisho hilo. Pia ndiye
    kiongozi wa Kamati ya Utendaji inayoshughulika na masuala ya kisera ya taasisi hiyo
    ya mpira nchini.
    Masuala ya kiutendaji yanashughulikuwa na Katibu Mkuu wa TFF. Kutokana na ukweli
    huo, kampeni zangu zitajikita zaidi kutangaza mambo ya kisera ya TFF, badala ya
    masuala ya kiutendaji.
    DIRA
    Kutengeneza fursa, uwezeshaji na furaha kupitia mpira wa miguu
    Dhima
    i. Kutengeneza na kusimamia miundombinu ya kutambua na kuendeleza vipaji vya
    wachezaji
    ii. Kuboresha mafunzo kwa ajili ya kupata makocha, madaktari wa michezo na
    waamuzi na watawala wa michezo kwa kiwango kikubwa cha ubora
    iii. Kusimamia utawala bora katika utendaji wa taasisi za michezo mkazo zaidi
    ukiwa wanachama wa TFF
    iv. Kusimamia vyombo vya kitaasisi vilivyopo ili viweze kufanya kazi kwa uhuru
    bila kuingiliwa.
    UFAFANUZI;
    Mafanikio katika mpira sio jambo la kufumba na kufumbua macho. Yanakuja baada
    ya kuweka misingi imara itakayosaidia kuchezeka kwa mpira.
    Misingi hii huchukua muda mrefu kuijenga na kuikamilisha. Nchini Tanzania
    changamoto kubwa naiona katika mfumo rasmi wa kutambua na kuendeleza
    wachezaji pamoja na heshima ya TFF kama taasisi makini inayosimamia mpira.
    Kutatua changamoto hizo kunaweza kuchukua miaka mingi, hivyo tunahitaji mpango
    endelevu, kama ilivyo katika utawala hapa nchini ambapo kuna Vision 2025 iliyoanza
    mwaka 1995.
    Kwa kuzingatia hilo, nimegawa sera zangu katika mipango ya muda mrefu na mfupi.
    Mipango ya muda mfupi ni ile nitakayoitekeleza ndani ya utawala wangu, wakati ile ya
    muda mrefu itakuwa mwendelezo wa Vision ya miaka 20 ijayo katika mpira wa miguu
    hapa nchini.
    A. MIPANGO YA MUDA MREFU
    1. KUTAMBUA VIPAJI
    Mchezaji wa mpira anatakiwa kuandaliwa kuanzia umri wa miaka 6. Katika umri huo
    watoto wa kitanzania wanakuwa shuleni.
    Kunatakiwa kuwapo mfumo rasmi wa kuwatambua wachezaji wakiwa wadogo. Kwa
    kuwa michezo imerudi shuleni tutaweka mpango endelevu wa kutoa mafunzo kwa
    walimu wa michezo shuleni, ili waweze kuwapa wanafunzi mafunzo stahili kwa umri
    wao.
    Pia mpango huo utaelezea mfumo rasmi ambapo walimu hawa watakuwa wanaripoti
    kwa mratibu wa mpira wa miguu wa mkoa. Huyu atakuwa ni mwajiriwa wa TFF.
    Ataripoti kwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF Makao Makuu.
    Atakuwa akiwasimamia walimu wa michezo shuleni, akiwa na lengo la kutambua
    wanafunzi wenye vipaji na atahifadhi kumbukumbu na takwimu kuhusu wachezaji
    hawa.
    Pia atatoa mapendekezo ya wanafunzi wanaostahili kupelekwa shule maalumu za
    vipaji vya mpira wa miguu ‘sports academy’.
    2. KUENDELEZA VIPAJI
    Baada ya kuwa na mfumo wa kutambua vipaji, sasa vipaji hivyo vinatakiwa
    kuendelezwa. Hapo ndipo tunapohitaji uwepo wa shule maalumu za vipaji vya
    michezo.
    Wanafunzi wenye vipaji vya mpira wa miguu wanatakiwa kuwekwa kwenye shule
    maalumu ili kupata muda wa kutosha kuendeleza vipaji vyao, lakini pia kuwa na
    miundombinu rafiki karibu nao.
    Kama taasisi tutaweka malengo ya kuwa na sports academy katika kanda sita. Kanda
    ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Ziwa
    na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
    Katika kipindi cha miaka 20 ijayo huu ndio uwe mkakati wetu. Lakini katika kipindi
    changu cha uongozi yaani miaka minne, nitahakikisha shule moja ya aina hiyo
    inajengwa kanda ya Kati Dodoma kwa ajili ya kuvipokea vipaji hivyo na kuviendeleza.
    Nitaalika serikali, mashirika ya umma na taasisi za watu binafsi kujenga shule hizo
    kwenye Kanda ambazo tumeziainisha ili kuweza kuwa na mfumo uliosambaa kwa
    usawa nchi nzima katika kuendeleza vipaji hivi.
    3. KUIMARISHA TFF KITAASISI
    Tunahitaji kuwa na taasisi imara na yenye kuheshimika machoni pa Watanzania na
    ulimwengu kwa ujumla, ili kushawishi wadau kujitoa katika kufadhili na kuendeleza
    michezo.
    Uongozi wa kaka yangu LeodegarTenga ulifanikiwa kujenga misingi ya kitaasisi ndani
    ya TFF.
    Kuendeleza msingi mzuri wa kitaasisi uliopo kwa kuhakikisha unafanya kazi
    inavyotakiwa. Mpira unabeba maslahi ya Watanzania wengi. Taasisi inayoongoza
    mpira inatakiwa kuongozwa kwa umakini na ufanisi mkubwa.
    B. MIPANGO YA MUDA MFUPI
    Katika kipindi changu cha miaka minne nimekusudia kufanya mambo muhimu kama
    ifuatavyo:-
    1. KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA AZIMIO LA BAGAMOYO
    Kusimamia utekelezaji wa Azimio la Bagamoyo katika maeneo makuu manne,
    *Taasisi za mpira na Utawala, Ufundi, Upatikanaji wa vifaa bora na Uhuru wa
    vyombo vya kikatiba.
    UTEKELEZAJI: -Nitasimamia kwa nguvu zote Road Map ya utekelezaji wa Azimio la
    Bagamoyo kwa kusisitiza masharti kwa klabu na vyama vya soka yatakayohakikisha
    Azimio la Bagamoyo linatekelezwa kwa vitendo,".
    SHIJA RICHARD SHIJA, MGOMBEA URAIS WA TFF, DAMU MPYA, MTAZAMO MPYA, MABADILIKO NI SASA.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TARAJIA HAYA KATIKA SOKA YA TANZANIA SHIJA RICHARD AKIWA RAIS WA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top