• HABARI MPYA

    Friday, August 11, 2017

    AZAM ‘WALIAMSHA DUDE’ KAMPALA...MGHANA APIGA ZOTE MBILI URA WAFA 2-0 KWAO

    Na Mwandishi Wetu, KAMPALA
    TIMU ya Aza FC imepata ushindi wa kwanza katika ziara yake Uganda kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuwachapa wenyeji, URA mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Phillip Omondi, Kampaa jioni jioni ya leo.
    Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alichezesha kikosi kingine cha pili katika mchezo huo na kuwapumzisha wachezaji walioanza kwenye mechi mbili zilizopita wakitoa sare zote 2-2 na Uganda Kombaini na 1-1 na KCCA.
    Mabao yote mawili ya Azam FC yamefungwa na mshambuliaji Yahaya Mohammed, moja katika kila kipindi cha mchezo huo, la kwanza akifunga dakika ya 19 kwa shuti kali nje ya eneo la 18 kabla ya kutupia jingine la aina hiyo dakika ya 47.
    Yahya Mohammed (aliyepiga magoti) akipongezwa na Joseph Mahundi baada ya kufunga leo

    Licha ya mabadiliko makubwa kikosini kwenye mchezo huo, bado timu hiyo ilionekana kucheza na kuwa imara kwenye eneo la ulinzi huku kipa Mwadini Ally, akifanya kazi kubwa baada ya kuokoa michomo mingi ya URA.
    Mara baada ya mchezo huo wa tatu wa kirafiki kwenye kambi ya timu hiyo nchini Uganda ambapo jana ikitoka sare ya bao 1-1 na mabingwa wa Uganda KCCA, Azam FC itashuka tena dimbani Jumapili ijayo kumenyana na Onduparaka, mtanange utakaofanyika Uwanja wa Nambole kuanzia saa 10.00 jioni.
    Ziara hiyo itahitimishwa Jumatatu ijayo kwa Azam FC kucheza mchezo wa tano wa kirafiki dhidi ya washindi wa tatu wa Ligi Kuu Uganda msimu uliopita, Vipers FC, utakaofanyika Uwanja wa St Marys uliopo Kitende, Uganda.
    Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa: Mwadini Ally, Swaleh Abdallah, Hamimu Karim, Abdallah Kheri, David Mwantika, Stephan Kingue, Idd Kipagwile/Braison Raphael dk57, Salmin Hoza/Frank Domayo dk84, Yahaya Mohammed/Yahya Zayd dk70, Enock Atta Agyei/Masoud Abdallah dk55 na Joseph Mahundi/Ramadhan Singano dk81.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM ‘WALIAMSHA DUDE’ KAMPALA...MGHANA APIGA ZOTE MBILI URA WAFA 2-0 KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top