• HABARI MPYA

    Sunday, July 09, 2017

    SIMBA YAMCHUKUA MBONDE ‘FASTA’ KUZIBA PENGO LA BANDA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Simba imemsajili beki wa Mtibwa Sugar, Salim Mbonde kwa mkataba wa miaka miwili kuziba pengo la Abdi Banda anayehamia Afrika Kusini.
    Mbonde amesaini saa chache baada ya kuwasili Dar es Salaam akitokea Afrika Kusini, ambako aliiongoza timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kushika nafasi ya tatu kwenye Kombe la COSAFA.
    Taarifa ya Simba SC imesema kwamba Banda amesaini mbele ya mfadhili wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’ Dewji ambaye kwa sasa anaihudumia timu kwa matumaini ya kuwa kuwa mmiliki wake atakapouziwa hisa baadaye. 
    Salim Mbonde (kushoto) akisaini mkataba wa kujiunga na Simba SC leo baada ya kuwasili kutoka Afrika Kusini

    Banda amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Baroka F.C ya Afrika Kusini baada ya kung’ara katika michuano ya Kombe la COSAFA Castle nchini Afrika Kusini akiiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu.
    Na wakati Banda anakwenda kuanza maisha mapya timu hiyo ya Ga-Mphahlele, karibu na Polokwane, Limpopo ambayo inacheza Ligi Kuu ya nchini humo, Simba imeona bora kumsanini ‘pacha wake’ Taifa Stars, Mbonde.
    Mbonde alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza michuano ya COSAFA Castle na kutwaa Medali ya Shaba baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa jana Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg.
    Kutoka na ushindi huo, Tanzania inaondoka na dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho wamepata dola 8,300.
    Fainali ya COSAFA Castle 2017 inachezwa leo Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng mjini Rusternburg baina ya majirani, Zambia na Zimbabwe na bingwa atapata dola 42,000 na mshindi wa pili dola 21,000.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAMCHUKUA MBONDE ‘FASTA’ KUZIBA PENGO LA BANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top