• HABARI MPYA

  Sunday, July 09, 2017

  MBARAKA YUSSUF ABAKI AFRIKA KUSINI KWA MATIBABU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI chipukizi wa Tanzania, Mbaraka Yussuf Abeid amebaki Afrika Kusini kwa matibabu kufuatia kuugua akiwa nchini humo na timu ya taifa lake, Taifa Stars kucheza michuano ya Kombe la COSAFA Castle.
  Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema leo asubuhi baada ya Taifa Stars kurejea Dar es Salaam kwamba Mbaraka amebaki Afrika Kusini kwa matibabu.
  “Ninamshukuru Mungu tumerudi salama nyumbani na safari yetu ilikuwa salama tangu tunaenda hadi tumerudi na hali za wachezaji ni nzuri isipokuwa Mbaraka Yussuf amebaki Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi,”alisema.
  Mbaraka Yussuf amebaki Afrika Kusini kwa matibabu baada ya kuugua kwenye Kombe la COSAFA
  Mbaraka sasa ana nafasi ndogo ya kujumuishwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kitakachomenyana na Rwanda Julai 14, mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza katika mchezo wa kwanza wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN). 
  Mbaraka alicheza mechi mbili tu kati ya mbili tu kati ya sita za Tanzaniaa kwenye Kombe la COSAFA, tena zote akitokea benchi, ya kwanza katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Malawi na katika sare ya 0-0 na Angola.
  Baada ya hapo akaumia na kushindwa kuendelea na mashindano, huku kocha Mayanga akimuongeza kikosini mshambuliaji mpya wa Simba, John Bocco kwa ajili yaa mechi dhidi ya Rwanda.
  Taifa Stars ilitwaa Medali ya Shaba kwenye Kombe la COSAFA baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa jana Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg.
  Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza ya Tanzania, kabla ya Nahodha Himid Mao, Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi kumtungua kipa wa Mamba Samuel Ketsekile kuipatia Taifa Stars ushindi mzuri wa 4-2.
  Kipa wa Tanzania, Said Mohammed Mduda alipangua ya nne ya Lesotho iliyopigwa na Nahodha wao, Thapelo Mokhehle kufuatia Sera Motebang kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani. Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle.
  Kutoka na ushindi huo, Tanzania inaondoka na dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho wamepata dola 8,300, wakati bingwa Zimbabwe amepata dola 42,000 na mshindi wa pili, Zambia dola 21,000.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBARAKA YUSSUF ABAKI AFRIKA KUSINI KWA MATIBABU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top