• HABARI MPYA

  Sunday, June 04, 2017

  NI REAL MADRID TENA ULAYA, RONALDO AKIFANYA VIBAYA KIBIBI KIZEE CHA TURIN

  Na Mwandishi Wetu, CARDIFF
  REAL Madird ya Hispania imefanikiwa kutetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Juventus ya Italia usiku huu Uwanja wa Millennium mjini Cardiff, Wales.
  Mwanasoka bora wa dunia, Mreno Cristiano Ronaldo amefunga mabao mawili, moja kila kipindi, huku mabao mengine yakifungwa na Casemiro na Marco Asensio na la Juve limefungwa na Mario Mandzukic kukamilisha msimu wa Ligi ya Mabingwa 2017.
  Hilo linakuwa taji la 12 la michuano hiyo kwa Real Madrid tangu inaitwa Klabu Bingwa Ulaya, baada ya awali kulitwaa katika miaka ya 1956, 1957, 1958, 1959, 1960, 1966, 1998, 2000, 2002, 2014 na 2016.

  Real Madrid wakishangilia na taji lao baada ya kukabidhiwa Uwanja wa Millennium mjini Cardiff leo 

  Chochote unachoweza kufanya, naweza kufanya vizuri? Ronaldo akijaribu kufunga bao kama la Mario Mandzukic, lakini mpira ukatoka nje  

  Na hiyo ndiyo klabu iliyotwaa mara nyingi zaidi taji hilo, ikifuatiwa na AC Milan ya Italia mara saba, Bayern Munich ya Ujerumani, Barcelona ya Hispania na Liverpool ya England zote mara tano kila moja.  
  Katika mchezo wa leo, Cristiano Ronaldo alianza kuifungia Real dakika ya 20 akimalizia pasi ya Daniel Carvajal – lakini bao hilo halikudumu, kwani Mandzukic aliisawazishia Juve dakika saba baadaye kwa tik tak akimalizia mpira wa Gonzalo Higuain.
  Timu hizo zikaenda kupumzika zikiwa zimefungana 1-1 na wakati kikitarajiwa kipindi kigumu cha pili, mambo yakawa mepesi kwa kocha Mfaransa mwenye asili yaq Algeria, Zinadine ZIdane baada ya timu yake kufanikiwa kuongeza mabao matatu.
  Alianza Casemiro dakika ya 61 kabla ya Ronaldo kufunga la tatu dakika ya 64 na Marco Asensio kumaliza kazi kwa bao la nne dakika ya 90.
  Juve ilimaliza pungufu, baada ya mshambuliaji wake, Juan Cuadrado aliyetokea benchi dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Andrea Barzagli kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 84 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano, kufuatia kumsukuma beki wa Real, Sergio Ramos.
  Mabao mawili ya leo yanamfanya Ronaldo aendelee kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa, akifikisha mabao 105 tangu 2003 alipoanza kucheza michuano hiyo akiwa Manchester United ya England. Na anafuatiwa na hasimu wake mkubwa, Muargentina Lionel Messi mwenye mabao 94 tangu mwaka 2005 akiwa na Barcelona. 
  Kikosi cha Real Madrid kilikuwa: Navas, Carvajal, Sergio Ramos, Varane, Marcelo, Kroos/Alvaro Morata dk89, Casemiro, Modric, Isco/ Marco Asensio dk82, Benzema/Bale dk77 na Ronaldo.
  Juventus: Buffon, Dani Alves, Barzagli/Cuadrado dk66, Bonucci, Chiellini, Alex Sandro, Pjanic/Marchisio dk70, Khedira, Higuain, Dybala/Lemina dk78 na Mandzukic.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI REAL MADRID TENA ULAYA, RONALDO AKIFANYA VIBAYA KIBIBI KIZEE CHA TURIN Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top