• HABARI MPYA

    Thursday, June 22, 2017

    TAIFA STARS WAONDOKA LEO KUFUATA KOMBE LA COSAFA

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kuondoka Saa 1:00 usiku wa leo kwenda Afrika Kusini tayari kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) Castle 2017.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika hoteli ya Urbun Rose, eneo la Kisutu, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema kwamba mazoezi maandalizi yalikuwa mazuri kwa ajili ya michuano hiyo na vijana wake wapo tayari kwa michauno hiyo.
    Mayanga alisema mchezaji pekee ambaye alizua hofu ni mshambuliaji chipukizi, Shaabani Idd Chilunda aliyeumia mazoezini, lakini taarifa za matabibu zinasema atacheza mashindano hayo.
    “Namshukuru mungu tumemaliza mazoezi salama leo asubuhi na tunatarajia kuondoka saa moja usiku kuelekea nchini Afrika Kusini, ambako tutafanya pia mazoezi ya siku mbili kabla ya kuanza kwa michuano,”amesema.
    Kwa upande wake, Daktari wa Taifa Stars, Gilbert Kigadye amesema kwamba itachukua siku tatu au nne ili Chilunda kupona na kuanza mazoezi.
    “Shaaban ameumia nyonga alipokuwa akiurukia mpira uliokuwa mbali na kupata maumivu hayo, ila bado tunamtibu na itachukua siku tatu au nne hadi arudi katika hali yake ya kawaida,”amesema Kigadye.
    Naye Nahodha wa timu hiyo, Himid Mao Mkami amesema kwamba kwa asilimia walikuwa na kipindi kizuri cha maandalizi kwa takriban wiki moja na kwa ujumla wamefanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo wa mwisho wakilazimishwa sare ya 1-1 na Lesotho wiki mbili ziliziopita.
    “Tunamshukuru Mungu tumemaliza salama mazoezi na hali zetu wote ni nzuri isipokuwa mwenzetu Shaaban ambaye aliumia mazoezini na kwa asilimia kubwa tumefanya mazoezi kwa kufuata kile tulichoelekezwa na mwalimu na nina imani tutafanya vizuri,”amesema.
    Michuano ya Kombe la COSAFA inatarajiwa kuanza Juni 25, mwaka huu na Tanzania imepangwa kundi A pamoja na Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B lina timu za Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. 
    Botswana, Zambia, Namibia, Lesotho na Swaziland na wenyeji, Afrika Kusini zitacheza mechi maalumu za mchujo kuwania kuingia robo fainali.
    Kikosi cha Taifa Stars ni makipa Aishi Salum Manula  (Azam FC), Benno David Kakolanya  (Yanga SC) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar FC). 
    Mabeki ni Shomary Salum Kapombe (Simba SC), Hassan Kessy (Yanga SC), Gardiel Michael (Azam FC), Hamim Abdulkarim (Toto Africans FC), Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Mbonde, (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons).
    Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Salmin Hoza wa Azam FC, Muzamil Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga SC), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Kichuya (Simba SC).
    Washambuliaji ni Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Yussuf (Azam FC), Stahmili Mbonde (Mtibwa Sugar), Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).
    Benchi la Ufundi linaundwa na Salum Mayanga, akisaidiwa na Fulgence Novatus, kocha wa makipa, Patrick Mwangata, Meneja Dani Msangi, Madaktari Gilberti Kigadiya na Richard Yomba pamoja na mtunza vifaa Ally Ruvu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS WAONDOKA LEO KUFUATA KOMBE LA COSAFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top