• HABARI MPYA

    Friday, June 23, 2017

    EVERTON ‘KUIPAISHA’ TANZANIA MECHI NA MAN UNITED ENGLAND

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Everton itavaa jezi zenye nembo iliyoandikwa Tembelea Tanzania katika mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Manchester United Januari.
    Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa kampuni ya SportPesa Tanzania, Tarimba Abass katika mkutano na Waandishi wa Habari leo kwenye hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam wakati wa kuzungumzia ziara ya klabu hiyo nchini.
    Everton yenye wachezaji nyota akiwemo Mbelgiji, Romelu Lukaku, itazuru Tanzania kucheza mechi ya kirafiki na Gor Mahia Julai 13, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    “Leo tumefungua rasmi ujio wa Everton hapa nchini na ujio huu una faida kubwa moja ambayo ni kuitangaza Tanzana katika Ligi ya England, ambapo watavaa jezi zenye nemba itakayoandikwa Visit Tanzania, ambayo tuna imani itatusaidia kupata watalii wengi katika nchini yetu,”amesema Tarimba.
    Tarimba Abbas (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kuhusu ujio wa Everton
    Mwenyekiti huyo wa zamani wa klabu ya Yanga, Tarimba amesema kwamba ujio huo utasaidia kuitangaza zaidi nchi yetu dunia nzima na kuifanya iendelee kutambulika zaidi kimataifa na kuvutia watalii zaidi kuja nchini.
    Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi alikuwepo kwenye mkutano huo na akaishukuru SportPesa kwa kusaidia kwoa michezo nchini.
    Everton inatarajiwa kuwasili nchini Julai 12 kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia, iliyopata nafasi hiyo baada ya kutwaa taji la mashindano ya wiki moja, SportPesa Super Cup mapema mwezi huu Dar es Salaam
    Michuano ya SportPesa Super Cup ilianza Juni 5 hadi 11 mjini Dar es Salaam, ikishirikisha timu za Simba SC, Yanga SC, Singida United na Jang'ombe Boys za Tanzania, Gor Mahia, AFC Leopards, Nakuru All Stars na Tusker FC za Kenya.
    Bingwa wa michuano hiyo, Gor Mahi aliyemfunga mpinzani wake wa Kenya, AFC Leopards 3-0 katika fainali Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam alipata pia dola za Kimarekani 30,000, zaidi ya Sh. Milioni 65.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: EVERTON ‘KUIPAISHA’ TANZANIA MECHI NA MAN UNITED ENGLAND Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top