• HABARI MPYA

    Thursday, June 22, 2017

    MAVUGO BADO YUPO YUPO SANA SIMBA, KABURU ASEMA HAACHWI NG’O

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MAKAMU wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema kwamba hawana mpango wa kumuacha mshambuliaji wao, Mrundi, Laudit Mavugo.
    Baada ya kusajiliwa John Bocco ‘Adebayor’ kutoka Azam FC, kurejeshwa kwa Mganda Emmanuel Okwi kuna wasiwasi kama watafanikiwa kumpata mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma kutoka Yanga, Simba wanaweza kumuacha Mavugo.
    Na kwa sababu hiyo imedaiwa Mavugo ameanza mipango ya kutafuta timu nyingine ya kujiunga nayo kuelekea msimu ujao.
    Lakini taarifa hizo zimepingwa na Kaburu, ambaye amesema Mavugo bado ni mchezaji wao na ana mkataba wa msimu mmoja zaidi kuendelea kufanya kazi Msimbazi.
    Simba imesema haina mpango wa kumuacha mshambuliaji wake, Mrundi, Laudit Mavugo

    “Mavugo ana mkataba na klabu na bado klabu haijapokea ofa yoyote kutoka popote ikimuhitaji Mavugo,”amesema Kaburu.  
    Simba inatamba katoka soko la usajili kwa sasa, ikiwa klabu inayosajili wachezaji wengi wakubwa kuliko wapinzani wake, Azam na Yanga.
    Hadi sasa tayari Simba imebomoa ngome ya Azam FC na kuwasajili wachezaji wake watatu tegemeo, mbali na aliyekuwa Nahodha, Bocco wengine ni ni kipa Aishi Manula na beki wa kulia, Shomary Kapombe. 
    Pamoja na hayo, Simba SC imewasajili kipa Emanuel Mseja, mabeki Jamal Mwambeleko kutoka Mbao FC, Yussuf Mlipili kutoka Toto Africans na Ally Shomary kutoka Mtibwa Sugar, huku pia ikiwa mbioni kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani, Mganda Emmanuel Okwi kutoka SC Villa ya kwao.
    Simba inafanya usajili wa kishindo, baada ya kufanikiwa kukata tiketi ya kurejea kwenye michuano ya Afrika mwakani kwa mara ya kwanza baada ya mitano.
    Wekundu hao wa Msimbazi watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, kufuatia kutwaa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Mei 27 mwaka huu kwa kuifunga Mbao FC 2-1 Uwanja wa Jamhuri, Dodoma. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAVUGO BADO YUPO YUPO SANA SIMBA, KABURU ASEMA HAACHWI NG’O Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top