• HABARI MPYA

    Thursday, June 22, 2017

    MSUVA AMLILIA ALLY YANGA AKIKUMBUKA KIROBA CHA MCHELE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WINGA wa Yanga SC, Simon Msuva amesema ameumizwa na kifo cha aliyekuwa shabiki mkubwa wa timu hiyo, Ally Mohammed ‘Ally Yanga’ aliyefariki dunia juzi Dodoma.
    “Kifo cha Ally Yanga kimeniuma sana, maana alikuwa ni zaidi ya shabiki kwangu, kwa sababu alikuwa ananiambia vitu vingi sana hasa katika soka letu la Tanzania. Kikubwa ambacho sitakuja kukisahau ni siku ambayo  alinikabidhi kiroba cha mchele Uwanja wa Taifa baada ya kumaliza mechi, kwa kweli sina mengi ya kuzungumzia juu ya Ally Yanga, ila imeniuma sana kumpoteza shabiki huyu mzalendo," amesema Msuva.
    Ally Yanga alifariki baada ya ajali ya gari akiwa kwenye msafara wa mbio za Mwenge kabla ya kupata ajali hiyo barabara ya Wiyenzele kuelekea Chipogoro na kufariki hapo hapo.
    Simon Msuva (kushoto) akiwa na kiroba alichopewa na marehemu Ally Yanga (kulia)

    Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Ally Yanga likiwasilishwa eneo la makuburini

    Ally aliyezaliwa mkoani Shinyanga Machi 1, mwaka 1984 katika familia ya watoto sita, kabla ya umauti wake inafahamika alikuwa anaishi Yombo Vituka, Dar es Salaam. Lakini amezikwa Shinyanga baada ya kuagwa jana Dodoma.
    Aliibukia Ubungo miaka ya nyuma kidogo ambako alikuwa anafanya shughuli ya kusajili laini za simu za mkononi katika vibanda vilivyokuwa pembeni ya kituo kikuu cha mabasi ya mikoani, Ubungo Terminal.
    Na alianza kuonekana Uwanja wa Taifa pamoja na kikundi cha mashabiki wa Yanga cha Ubungo Terminal, ambako ndipo lilipokuwa tawi lake.
    Lakini tangu baada ya uchaguzi Mkuu Novemba 2015, Ally Yanga ameadimika viwanja vya soka kutokana na kujikita zaidi kwenye shughuli za Chama cha Mapinduzi CCM.
    Ally hakuwa shabiki wa Yanga tu, enzi za uhai wake alikuwa akizishabiki pia timu za taifa, kuanzia za vijana na wakubwa za wanawake na wanaume. 
    Alikuwa maarufu Afrika Mashariki kutokana na kwenda kuishabikia Taifa Stars kwenye mechi za Kombe la CECAFA Callenge nchi za Kenya na Uganda. Lakini pia amewahi kusafiri hadi nje ya Afrika ya Afrika Mashariki akiwa na Taifa Stars kwenye mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika na Kombe ka Dunia. Mungu ampumzishe kwa amani Ally Yanga. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA AMLILIA ALLY YANGA AKIKUMBUKA KIROBA CHA MCHELE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top