• HABARI MPYA

    Friday, June 23, 2017

    TAIFA STARS YAFIKA SALAMA, KUANZA NA MALAWI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha wachezaji 22 wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kimesafiri na kufika salama nchini Afrika Kusini kikitokea Dar es Salaam, Tanzania.
    Timu hiyo iliyoondoka jana Alhamisi Juni 22, 2017 kwenda Afrika Kusini kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda, itakuwa huko kwa ajili ya michuano ya kuwania Kombe la Castle Cosafa.
    Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti, itaanza kampeni za kucheza hatua ya Robo fainali kwa kucheza na Malawi Jumapili, Juni 25, mwaka huu katika michuano hiyo iliyoandaliwa na Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa).
    Taifa Stars itamkosa Nahodha wake, Mbwana Samatta kwenye michuano ya COSAFA

    Tanzania si mwanachama wa Cosafa, lakini imealikwa katika mashindano hayo na imepangwa kundi A na timu za Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. Kinara wa kila kundi atakwenda moja kwa moja hatua ya robo fainali.
    Timu za Botswana, Zambia na Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na Swaziland tayari zimepangwa hatua ya robo fainali hivyo zinasubiri vinara wawili kutoka makundi ya A na B kuungana nazo kucheza robo fainali.
    Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Shabani Mayanga, amesema kwamba anaichukulia michuano hiyo kwa umakini na uzito mkubwa kwa wachezaji kuzidi kupata uzoefu wa mechi nyingi za kimataifa kwa mwaka.
    Kadhalika, kiufundi Mayanga anachukulia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi makubwa ya mchezo dhidi ya Rwanda wa kuwania kucheza nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani - CHAN.
    Mchezo huo wa kwanza utafanyika Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
    Kikosi cha Taifa Stars kilichopo Afrika Kusini kinaundwa na makipa Aishi Salum Manula  (Azam FC), Benno David Kakolanya  (Young Africans SC) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar FC). 
    Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Salum Kapombe    (Azam FC) na Hassan Hamis Ramadhan ‘Kessy’ (Young Africans SC) wakati upande wa kushoto wapo Gadiel Michael (Azam FC) na Hamim Abdulkarim (Toto Africans FC).
    Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Hassan Abdallah (Mtibwa Sugar), Abdi Hassan Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) wakati viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao Mkami (Azam FC) na Salmin Hoza wa Mbao FC.
    Kadhalika wako viungo wa kushambulia ambao ni Mzamiru Yassin Selembe (Simba), Simon Happygod Msuva (Young Africans SC), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Ramadhani Kichuya (Simba SC).
    Katika safu ya ushambuliaji wamo Thomas Emmanuel Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Abeid Yusufu (Kagera Sugar), Stamili Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YAFIKA SALAMA, KUANZA NA MALAWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top