• HABARI MPYA

    Saturday, June 24, 2017

    MTAA DAR WAPEWA JINA LA KIUNGO WA SPURS, WANYAMA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa kimataifa wa Kenya, Victor Mugubi Wanyama anayechezea Tottenham Hotspur ya England amepewa heshima kubwa Tanzania baada ya mtaa uliokuwa unajulikana kama Viwandani eneo la Shekilango, Dar es Salaam kupewa jina lake.
    Mtaa wa Viwandani uliopo kata ya Shekilango, Manispaa ya Ubungo sasa utakuwa unajulikana kama Mtaa wa Victor Wanyama.
    Hiyo inafuatia ziara ya kiungo huyo wa klabu ya Tottenham Hotspur ya England nchini, ambayo ilimfikisha hadi studio za Azam TV ambako alikutana na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Yussuf Bakhresa.
    Wanyama yupo nchini kwa siku tatu sasa kwa ajili ya mapumziko yake binafsi na amepata bahati ya mapokezi mazuri kutoka kwa Yussuf Bakhresa, ambaye kampuni yake inamiliki pia klabu ya Azam FC ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    Victor Wanyama akiwa na mkurugenzi wa Azam TV, Yussuf Bakhresa leo Dar es Salaam
    Mtaa wa Viwandani kuanzia sasa utakuwa unaitwa Mtaa wa Victor Wanyama


    Victor Wanyama akiwa na Yussuf Bakhresa ofisi za Azam TV, Tabata, Dar es Salaam
    Wanyama akiwa na Mtendaji Mkuu wa Azam TV, Tido Mhando na mabosi wengine wa kampuni hiyo

    Leo mchana alikuwa studio za Azam TV, Tabata, Dar es Salaam ambako alikutana na wakuu na wafanyakazi wa kampuni hiyo na kufurahi nao.  Ni kijana mcheshi, asiye hata na dalili za majivuno ambaye alimchangamkia kila mtu bila kujali hali wala mwonekano wake. 
    Amefanya mahojiano na Waandishi wa Habari mbalimbali nchini na amekuwa mwepesi kumjibu yeyote chochote. Anazungumza Kiswahili fasaha wakati wowote bila hata kuonyesha dalili za kwamba anafanya hivyo kwa tabu kwa sababu amekaa Ukaya kwa muda sasa.
    Kihistoria, Wanyama aliyezaliwa Juni 25, mwaka 1991 alisoma shule ya Kamukunji  na kisoka aliibukia akademi ya JMJ kwao, kabla ya kuchezea klabu za Nairobi City Stars na AFC Leopards katika Ligi Kuu ya Kenya.
    Mwaka 2007 alijiunga na Allsvenskan ya Helsingborg nchini Sweden, lakini akalazimika kuondoka baada ya kaka yake, McDonald Mariga kwenda Parma ya Italia mwaka 2008 na Wanyama akarejea Kenya.
    Baadaye akaenda kufanya majaribio Beerschot AC ya Ubelgiji na kufuzu, hivyo kusaini mkataba wa miaka wa minne kuanza kucheza rasmi Ulaya mwaka 2008, kabla ya mwaka 2011 kununuliwa na Celtic ya Ligi Kuu ya Scotland.
    Mwaka 2013 alinunuliwa na Southampton ya England kwa dau la Pauni Milioni 12.5 na kuwa Mkenya wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England. Baada ya mechi 85 akifunga mabao manne, Wanyama akanunuliwa na Tottenham Hotspur mwaka jana kwa dau la Pauni Milioni 11 na msimu huu ameiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu, nyuma ya Chelsea walioibuka mabingwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTAA DAR WAPEWA JINA LA KIUNGO WA SPURS, WANYAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top