• HABARI MPYA

    Sunday, June 25, 2017

    NYAMLANI AJITOA MBIO ZA URAIS WA TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAKAMU wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani amejitoa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais wa shirikisho hilo unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
    Taarifa ya Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas imesema kwamba Nyamlani amewasilisha barua leo Jumapili Juni 25, mwaka huu ikiwa ni siku moja tu tangu Kamati ya Uchaguzi ipitishe jina lake kuwa miongoni mwa wagombea 10 wanaowania nafasi hiyo ya urais. Sababu aliyoeleza ni masuala binafsi.
    Kwa msingi huo, wagombea wanaobaki kwenye kinyang’anyiro na kuhitajika kufika kwenye usaili kuanzia Juni 29, mwaka huu ni tisa wakiongozwa na Rais wa sasa, Jamal Malinzi anayetetea nafasi.
    Athumani Nyamlani (kulia) amewasilisha barua ya kujitoa kwenye uchaguzi wa TFF leo

    Mbali ya Malinzi wengine wanaowania nafasi hiyo ni Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe.
    Waliojitokeza kuwania Makamu wa Rais na kurejesha fomu wako Mulamu Ng’hambi, Michael Wambura, Geofrey Nyange, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.
    Mbali ya nafasi za urais na makamu rais, Abdallah Mussa - aliyekuwa akiwania nafasi ya kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji TFF kutoka Kanda Na. 1 (Mikoa ya Kagera na Geita) aliondolewa kwa sababu ya kutoambatanisha kivuli cha cheti ya elimu ya sekondari.
    Ikumbukwe Nyamlani alikuwa Makamu wa Rais wa TFF, chini ya Rais Leodegar Chilla Tenga kati ya Desemba 14, mwaka 2008 na Oktoba 27, mwaka 2013.
    Akawa mpinzani mkuu wa rais wa sasa wa TFF, Jamal Emil Malinzi katika uchaguzi uliopita Oktoba 27, mwaka 2013, lakini akashindwa baada ya kupata kura kura 52 dhidi ya 72 za ‘mbabe wake’.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NYAMLANI AJITOA MBIO ZA URAIS WA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top