• HABARI MPYA

    Tuesday, June 20, 2017

    AZAM WALALAMIKA ‘KUCHEZEWA RAFU’ USAJILI WA MBARAKA

    Na Shekha Jamal, DAR ES SALAAM
    AZAM FC imelalamika mshambuliaji wake mpya, Mbaraka Yussuf Abeid kubambikiwa mkataba feki ili kukwamisha mpango wake wa kuondoka Kagera Sugar.
    Taarifa ya Azam FC, imesema Mbaraka leo alikwenda ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchukua nakala ya mkataba wake, lakini akapewa mikataba miwili tofauti.
    “Pamoja na kwamba, sisi kama Azam tulikuwa na nakala halisi ambayo iliwasilishwa TFF kwenye usajili ulioisha. Lakini tulimwambia Mbaraka akachukue nakala yake TFF. Cha kustaajabisha ni kwamba, leo hii TFF imempatia mbaraka nakala mbili za mkataba ambazo moja inaonyesha mkataba uliosainiwa ni wa mwaka mmoja na mwingine ambao umefojiwa ukionyesha ni wa miaka mitatu,” imesema taarifa ya Azam.
    Azam FC imelalamika kuchezewa mchezo mchafu katika usajili wa Mbaraka Yussuf Abeid 

    “Mkataba mmoja umesainiwa tarehe 20 June 2016 na mwingine ukiwa ni wa tarehe 10 Agosti 2016.  Mkataba wa tarehe 20 June, umesainiwa ukionyesha mwaka mmoja na ule wa 10 Agosti ni 2016 ni miaka mitatu. Ukiacha tofauti ya miezi mitatu ya kusainiwa mikataba hii, lakini hata kiwango cha usajili ni tofauti mno,”.
    “Hata hivyo, mkataba wa miaka mitatu, umesainiwa bila kuwa na saini ya mchezaji, wala muhuri wa klabu ya Kagera Sugar n ahata jina la Mchezaji kwenye sehemu ya kusaini halijaandikwa.
    Tutaiweka hadharani mikataba hii kwa idhini ya mchezaji ili familia ya mpira ione mikataba yote miwili na kisha tarataibu nyingine zifuate,”.
    “Kuna uhuni mwingi ambao unafanywa kwenye baadhi ya mambo kwenye mpira wetu, hasa masuala ya mikataba ya wachezaji, Sisi Azam tunataka kulimaliza tatizo hili. Na kwa hili tutatumia wanasheria wetu kuwafikisha mahakamani wote walioshiriki kufoji mkataba wa Mbaraka ili kujenga precedent nzuri huko mbele,”imesema taarifa hiyo.
    Aidha, Azam FC imeiomba Kagera Sugar, ama kukanusha au kuthibitisha juu ya mikataba hiyo ili hatua stahiki zifuate, kwani suala la kufoji mikataba ya wachezaji ni uhuni ambao haupaswi kuchwa kuendelea kwenye soka ya Tanzania.
    Mbaraka amesaini mkataba wa miaka miwili wiki iliyopita kujiunga na timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, akitokea Kagera Sugar ya Bukoba, ambayo nayo ilimtoa Simba SC.
    Mchezaji huyo aliyeibukia timu ya vijana ya Simba, alishika nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akifunga mara 12 na kuzidiwa bao moja na wote, Simon Msuva wa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting waliofungana na kubeba pamoja kiatu cha dhahabu.
    Lakini katika sherehe za kuhitimisha msimu wa VPL, Mbaraka akatunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Ligi Kuu akiwaangusha Shaaban Iddi wa Azam FC na Mohammed Issa ‘Banka’ wa Mtibwa Sugar.   
    Mfungaji huyo wa bao la ushindi la Taifa Stars, ikiilaza 2-1 Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Machi 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, alizaliwa Septemba 2 mwaka 1997, Kinondoni, Dar es Salaam na akasoma Shule ya Msingi Kumbukumbu na baadaye sekondari ya Tabata kabla ya kuhamia Kinondoni Muslim alikohitimu Kidato cha Nne.
    Kinondoni Muslim ndiko haswa alikoanzia kucheza soka hadi mwaka 2014 alipokwenda kujiunga na timu ya vijana ya Simba SC ambako alicheza hadi 2015 akapandishwa timu ya kwanza chini ya kocha Muingereza, Dylan Kerr lakini wakati Ligi Kuu inakaribia kuanza akatolewa kwa mkopo Kagera Sugar.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM WALALAMIKA ‘KUCHEZEWA RAFU’ USAJILI WA MBARAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top