• HABARI MPYA

    Tuesday, June 27, 2017

    NGOMA HUYOOO AFRIKA KUSINI, ASAINI MIAKA MITATU POLOKWANE CITY

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Dombo Ngoma amehitimisha miaka yake miwili ya kucheza Yanga ya Tanzania, baada ya kukamilisha uhamisho wake kwenda Polokwane City ya Afrika Kusini.
    Kwa mujibu wa Polokwane, Ngoma mwenye umri wa miaka 27 sasa, amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na timu hiyo ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini baada ya kufuzu vipimo vya afya. 
    Na Ngoma anajiunga na timu hiyo iliyofuzu michuano ya MTN8 kama mchezaji huru, baada ya kumaliza mkataba wake Yanga ya Tanzania mwezi huu.
    Na baada ya kumpata Ngoma, Polo City inawatema kiungo Tlou Segolela na mkongwe Esau Kanyenda.
    Ngoma alikuwa na msimu wa kwanza mzuri Yanga SC, akiiongoza kutwaa mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) na kuiwezesha pia kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ua kutolewa 16 Bora Ligi ya Mabingwa.
    Hata hivyo, msimu wake wa pili Ngoma hakuwa mzuri Yanga kutokana na kusakamwa na maumivu ya goti, huku timu yake ikiweza tu kutetea taji Ligi Kuu na kuvuliwa mengine ya Ngao ya Jamii iliyochukuliwa na Azam na ASFC lililobebwa na Simba.
    Na hata katika michuano ya Afrika, Yanga haikuweza kurudia mafanikio yake ya msimu uliopita baada ya kushindwa kufuzu hatua ya makundi.
    Ngoma aliyezaliwa Kwekwe, Zimbabwe alijiunga na Yanga SC mwaka 2015 akitokea FC Platinum ya kwao, aliyoanza kuichezea mwaka 2012 akitokea Monomotapa United iliyomuibua mwaka 2011.
    Amewahi kuitwa timu ya taifa ya Zimbabwe mara kadhaa tangu mwaka 2011na hadi sasa amecheza mechi nane na kufunga mabao matatu.
    Na anakwenda Afrika Kusini, huku nchini Tanzania kukiwa kuna habari anakuja kesho kujiunga na mahasimu wa Yanga, Simba. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGOMA HUYOOO AFRIKA KUSINI, ASAINI MIAKA MITATU POLOKWANE CITY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top