• HABARI MPYA

    Thursday, June 29, 2017

    MALINZI ‘ACHINJWA KIAINA’ UCHAGUZI TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NI miujiza tu inasubiriwa ili kumnusuru Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi arejee kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa shirikisho hilo uliopangwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma.
    Hiyo inafuatia kunyimwa dhamana na kupelekwa mahabusu hadi Julai 3, mwaka huu kufuatia kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
    Hakimu mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Wilbord Mashauri amesema kwamba hatawapa dhamana hadi atakapoamua kuhusu suala hilo la kufuatia mabishano ya kisheria ya mawakili wa utetezi dhidi ya mawakili wa upande wa Serikali.


    Rais wa TFF, Jamal Malinzi akipelekwa mahabusu pamoja na Katibu wake, Selestine Mwesigwa na viongozi wa Simba

    Katika mashitaka hayo, 25 yamekwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
    Kutokana na kupelekwa Rumande hadi Julai 3 na iwapo Makahama haitabatilisha uamuzi wake wa kuwanyima dhamana, maana yake Malinzi hataweza kushiriki uchaguzi wa TFF, kutetea nafasi yake baada ya miaka yake minne ya awali.
    Hiyo ni kwa sababu hatashiriki zoezi la usajili wa wagombea, lililoanza jana na linatarajiwa kumalizika keshokutwa jioni.
    Baada ya kazi nzuri katika miaka yake minne ya mwanzo, Malinzi amechukua fomu kutetea nafasi yake dhidi ya Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe, baada ya mgombea mmoja, Athumani Nyamlani aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa TFF kujitoa.
    Nyamlani aliwasilisha barua ya kujitoa Juni 25, mwaka huu ikiwa ni siku moja tu tangu Kamati ya Uchaguzi ipitishe jina lake kuwa miongoni mwa wagombea 10 wanaowania nafasi hiyo ya urais. 
    Waliojitokeza kuwania Makamu wa Rais na kurejesha fomu wako Mulamu Ng’hambi, Michael Wambura, Geofrey Nyange, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.
    Malinzi amefanya kazi nzuri katika miaka yake minne ya awali, ikishuhudiwa kwa mara ya kwanza timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ikifuzu kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Mei mwaka huu nchini Gabon.
    Katika kipindi chake hicho, imeshuhudiwa michuano ya Kombe la TFF ikirejea, Ligi Kuu za Vijana na Wanawake zikianzishwa na mashindano yote yakiwa na udhamini.
    Mfumo wa Ligi za chini umeboreshwa na amedhibiti upangaji wa matokeo na mianya yake – mwaka jana akichukua maamuzi magumu ya kutengua matokeo yenye ‘harufu ya upangwaji’ ya Ligi Daraja za Kwanza na kuziadhibu timu zilizohusika, huku timu iliyofuatia ambayo haikufuzu, Mbao FC ya Mwanza ikichukua nafasi ya kwenda Ligi Kuu.
    Na ikashuhudiwa Mbao FC ikionyesha ushindani katika Ligi Kuu hadi kufika fainali ya Kombe la TFF, ambako ilifungwa kwa mbinde na Simba 2-1.   
    Japo kuna sehemu kama binadamu, Malinzi alikosea, lakini ‘mizani’ ya utendaji wake TFF inaegemea kwenye mazuri, maana yake soka ya Tanzania bado inamhitaji sana.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI ‘ACHINJWA KIAINA’ UCHAGUZI TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top