• HABARI MPYA

  Sunday, June 04, 2017

  TFF INAJUA KUNA KUPOKONYWA UENYEJI WA AFCON WA U-17?

  RASMI Tanzania itaandaa Fainali za kwanza za michuano ya Afrika, kufuatia kupewa uenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.
  Katika kilele cha mashindano ya U-17 mwaka huu nchini Gabon, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad aliitambulisha rasmi Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali zijazo za michuano hiyo.
  Ahmad alimkabidhi bendera ya CAF, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwesigwa Selestine mjini Libreville, baada ya fainali Uwanja wa l'Amitié Sino-Gabonaise.
  Mali ilishinda 1-0 dhidi ya Ghana, bao pekee la Mamadou Samake dakika ya 22 na kutwaa taji hilo kwa mara ya pili mfululizo.
  Vizuri Tanzania ilipata nafasi ya kushiriki fainali za kwanza za U-17 mwaka huu nchini Gabon na kuishia hatua ya makundi.
  Tanzania ilikuwa Kundi B pamoja na Mali na Niger zilizofuzu Nusu Fainali na pia kujikatia tiketi ya Kombe la Dunia la U-17 nchini India Oktoba mwaka huu na Angola iliyotolewa mapema pia.
  Serengeti Boys ilianza michuano kwa sare ya 0-0 na mabingwa watetezi, Mali kabla ya kwenda kushinda 2-1 dhidi ya Angola na kumaliza kwa kufungwa 1-0 na Niger kwa bao la utata hivyo kutolewa.
  Lilikuwa bao la utata, kwa sababu mfungaji aliuchukua mpira ambao ulikuwa umekwishatoka nje na kuurudisha uwanjani kwenda kufunga, wakati wachezaji wa Tanzania wameduwaa.
  Kipigo hicho kikaifanya Serengeti Boys ilingane kwa pointi na wastani wa mabao na  Niger hivyo kigezo cha mechi baina yao kuamua nani asonge mbele.
  Baada ya uzoefu huo iliyojipatia Gabon, viongozi wa TFF wanarudi Tanzania kuanza maandalizi ya fainali za mwaka 2019.
  Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikuwepo Gabon pamoja na Mshauri wake wa Ufundi, Pellegrinius Rutayuga mbali ya Katibu Mwesigwa.
  Na wote walijionea namna ambavyo Gabon walifanikiwa katika kuandaa mashindano hayo, ambayo kwao yalikuwa ya pili mfululizo baada ya mapema Januari mwaka huu kuwa wenyeji wa Fainali za wakubwa za Mataifa ya Afrika.
  Katika salamu zake za shukrani kwa Watanzania walioichangia Serengeti Boys kwenye ushiriki wake wa fainali za mwaka huu,  Malinzi alisema tusikubali kuwa wenyeji kama Gabon, ambao walivurunda.
  Gabon ilifungwa mechi zote na kutolewa hatua ya makundi tu kutoka Kundi A, walipokuwa na Ghana, Guinea na Cameroon.
  Unaweza ukasema kwa sababu labda walikurupushwa kuwa wenyeji kuipokea Shelisheli, lakini hata kwenye fainali za wakubwa Januari, Gabon ilitolewa hatua ya makundi pia.
  Tuseme Gabon pamoja na kuwa na wachezaji wanaocheza Ulaya, akiwemo Pierre-Emerick Aubameyanga wa Borussia Dortmund, bado wana kazi ya kupandisha soka yao.
  Wakati Malinzi na TFF wanafurahia uenyeji wa AFCON ya U-17 mwaka 2019, mimi ninataka niwakumbushe jambo moja, Gabon hawakuwa wateule halisi wa kuandaa fainali za U-17 mwaka huu.
  Nchi iliyoteuliwa kuwa mwenyeji wa AFCON ya U-17 mwaka huu ni Shelisheli, ambayo ilipanga kuyafanya kuanzia Aprili 2 hadi 16 April mwaka huu.
  Pamoja na hayo, Kamati ya Utendaji ya CAF wakati huo chini ya rais wake wa zamani, Issa Hayatou wa Cameroon ikawapokonya uenyeji Shelisheli baada ya ripoti ya wakaguzi wake kuonyesha mambo hayajaakaa sawa huko.
  Ilionekana Shelisheli hawajakamilisha maandalizi na ili kuepuka aibu ya maandalizi mabovu, CAF ikaiteua Gabon katika kikao chake cha Februari 3, mwaka 2017.
  Gabon wakaweka rekodi nzuri ya kufanya mashindano mawili makubwa mfululizo kwa ufanisi mkubwa kati ya Mei 14 hadi 28 mwaka 2017.
  Nataka niwaambie TFF, kupewa uenyeji si maana yake tayari wamejihakikishia kwamba fainali za U-17 mwaka 2019 zitafanyika.
  Fainali hizo zitafanyika tu iwapo maandalizi yake yatakuwa mazuri na kuiridhisha Kamati ya Ukaguzi ya CAF, vinginevyo na sisi tutapokonywa uenyeji kama Shelisheli.
  Kihistoria Tanzania tumezoea maandalizi ya zimamoto, au ya lala salama ambayo kwa kweli kama tutaendelea nayo kuna wasiwasi tukakwama.
  Maana yake tunapaswa kubadilika na TFF wakahakikisha mipango ya maandalizi ya fainali hizo inafanyika mapema na kwa ufasaha, kwa kuitumia Gabon kama kioo chao. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF INAJUA KUNA KUPOKONYWA UENYEJI WA AFCON WA U-17? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top