• HABARI MPYA

    Saturday, April 08, 2017

    UEFA YAMTABIRIA MAKUBWA MBWANA SAMATTA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Ulaya (UEFA) limemtaja mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta kama mmoja wa wachezaji wa kutazamwa kwa sasa barani humo.
    Katika ukurasa wake wa Twitter, UEFA imeandika; “Mchezaji wa kutazamwa? Mbwana Samatta amefunga mabao sita katika mechi zake tano zilizopita kwa Genk,”.
    Na wasifu huu unakuja wakati Genk inajitayarisha na mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Europa League dhidi ya wenyeji, Celta Vigo Alhamisi wiki ijayo Uwanja wa Balaidos.  
    Tayari Nahodha huyo wa Tanzania amekwishaweka wazi tamaa yake kucheza Ligi Kuu ya England na Manchester United ni sehemu anayotaka zaidi kwenda.
    UEFA imemtabiria makubwa mshambuliaji wa Genk, Mbwana Samatta
    United pia wamefuzu Nane Bora ya Europa League na wao Aprili 13 watakuwa wageni wa Anderlecht Uwanja wa Constant Vanden Stock, Ubelgiji.
    Na kwa sababu kocha wa United, Jose Mourinho anasaka mshambuliaji mwenye kipaji cha kufunga, basi Samatta anaweza kutimiza ndoto zake iwapo za kutua Old Trafford atamvutia Mreno huyo.
    Hadi sasa Samatta amekwishafunga mabao 18 katika mechi 49 alizoichezea Genk tangu asajiliwe Januari mwaka jana akitokea TP Mazembe ya DRC.
    Kati ya mechi hizo 49, michezo 18 Samatta alicheza msimu uliopita na 31 msimu huu na kati ya hiyo, ni michezo 30 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na 20 msimu huu.
    Mechi 19 kati ya hizo alitokea benchi, nane msimu uliopita na 11 msimu huu, wakati 11 hakumaliza baada ya kutolewa, tano msimu uliopita na sita msimu huu na katika mabao hayo 18, 12 amefunga msimu huu na sita msimu uliopita.
    Usiku huu, Samatta anatarajiwa kuichezea Genk katika mchezo wa kuwania kucheza michuano ya Europa League msimu ujao dhidi ya wenyeji, SV Roeselare Uwanja wa Schiervelde mjini Roeselare.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UEFA YAMTABIRIA MAKUBWA MBWANA SAMATTA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top