• HABARI MPYA

    Friday, April 21, 2017

    SIMBA WATAKA KUFANYA MAANDAMANO MAKUBWA DAR JUMANNE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Simba SC, Evans Aveva amemuandikia barua Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Simon Sirro kuomba kufanya maandamano ya amani kupinga kile wanachoamini uonevu wanaofanyiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). 
    Katika barua hiyo, ambayo nakala yake imetumwa pia kwa Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Aveva amesema kwamba wanataka waandamane Jumanne ya Aprili 25, mwaka huu.
    Aveva amesema wanataka maandamano hayo yatakayohusisha wanachama wote wa Simba, yaanzie makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi hadi Wizara ya Habari.
    Pointi tatu, mabao matatu; Rais wa Simba ameomba kibali cha maandamano Jumanne Dar es Salaam
    Barua ya Simba kwenda Kamanda wa Polisi Kanda Maalum mjini Dar es Salaam

    “Lengo la maandamano hayo ni kupeleka ujumbe kwa shirikisho hilo, ambalo limekuwa likifanya uonevu katika maamuzi yake dhidi ya klabu ya Simba. Ifahamike kuwa malalamiko mengi ya klabu ya Simba yamekuwa hayasikilizwi kwa kipindi kirefu,”amesema Aveva.
    Lakini pia Aveva amesema wana taarifa Msemaji wao, Hajji Manara ameitwa kwenye Kamati ya Maadili kwa kile kinachoonekana kutaka kumfungia na kumziba mdomo ili asiweze kuongeela uonevu huu.
    “Ni matumaini yetu kuwa jeshi lako litatoa ulinzi wa kutosha kwa wanachama na mashabiki wetu,”amesema Aveva katika barua yake hiyo kwenda kwa Kamanda Sirro.  
    Maombi hayo yanakuja muda mfupi baada ya TFF kumtaka Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Sunday Manara kufika Kamati ya Maadili Aprili 21, 2017 kujibu tuhuma za utovu wa nidhamu dhidi ya viongozi wa Shirikisho hilo.
    Yote haya yanafuatia wasiwasi wa kupokonywa pointi za mezani na Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ambazo walipewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 kutokana na malalamiko yao dhidi ya Kagera Sugar kumchezesha beki Mohammed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    Na hiyo ni baada ya Kagera Sugar kupinga uamuzi wa Kamati ya Saa 72 kuipa Simba SC kwa madai Fakhi alionyeshwea kadi ya njano katika mchezo wa Jumatano ya Januari 18, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kati ya wenyeji Kagera Sugar na African Lyon ya Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WATAKA KUFANYA MAANDAMANO MAKUBWA DAR JUMANNE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top