• HABARI MPYA

    Sunday, April 23, 2017

    AZAM FC YAILAZA 2-0 AFRICAN LYON KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki, Azam FC, imefanikiwa kuichapa African Lyon mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika usiku huu ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Mchezo huo ulioathiriwa na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia asubuhi, ulikuwa ni maalum kwa ajili ya benchi la ufundi la Azam FC kukipima kikosi chake na kuwaweka wachezaji kwenye ushindani kutokana na kutokuwa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) wikiendi hii.
    Mabao pekee ya Azam FC yameweka kimiani kiufundi na beki wa kulia, Erasto Nyoni, dakika ya 23 aliyefunga bao lake la pili kwenye mechi ya pili mfululizo, jingine akifunga katika ligi wiki iliyopita timu hiyo ilipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Ruvu.
    Nahodha wa Azam FC, Himid Mao (kulia) akimiliki mpira pembeni ya mchezaji wa African Lyon jana

    Bao jingine la mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu huu usiku huu lilifungwa na kiungo Mudathir Yahya, dakika ya 87 aliyemalizia kazi nzuri na winga Enock Atta Agyei, ambaye ni mmoja wa wachezaji walioonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo.
    Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Azam FC Aristica Cioaba, alipata fursa ya kuwatumia kwa mara ya kwanza wachezaji wake watatu waliokuwa majeruhi, mabeki Aggrey Morris, Yakubu Mohammed na kiungo Stephan Kingue, ambao aliwachezesha kwa dakika 55 kabla ya kuwafanyia mabadiliko.
    Pia aliwajumuisha kikosini wachezaji wanne wa timu ya vijana ya Azam FC, mabeki Abbas Kapombe, Said Mohamed, pamoja na kiungo Stanslaus Ladislaus na mshambuliaji Yahaya Zaidi, ambao wawili hao walicheza dakika saba za mwisho.
    Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho kabla ya Jumatatu kuanza mandalizi ya kujiandaa na mchezo ujao wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) utakaofanyika wikiendi ijayo huku timu itakayopangiwa nayo ikitarajia kujulikana kesho Jumapili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAILAZA 2-0 AFRICAN LYON KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top