• HABARI MPYA

    Sunday, April 30, 2017

    MBAO WAIFUATA SIMBA FAINALI KOMBE LA TFF

    Na Mwandishi Wetu, MWANZA
    YANGA imevuliwa taji la pili msimu huu, baada ya kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inayojulikana kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kufuatia kipigo cha 1-0 kutoka kwa Mbao FC katika mchezo wa Nusu Fainali jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. 
    Mapema mwanzoni mwa msimu, Yanga ilivuliwa taji la Ngao ya Jamii baada ya kufungwa na Azam FC kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya 1-1 katika mchezo wa kuashiria ufunguzi wa msimu mpya, Agosti 17, mwaka jana. 
    Na sasa Yanga ina jukumu la kutetea taji lake moja lililobaki na kubwa zaidi, la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ambako wanakabana koo na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
    Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Erick Onoka wa Arusha, aliyesaidiwa na Julius Kasitu na Mdogo Makame wa Shinyanga hadi mapumziko, tayari Mbao walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.
    Ni Yanga wenyewe waliojifunga bao hilo dakika ya 27, baada ya beki wake, Andrew Vincent ‘Dante’ kuunganishia nyavuni kwake krosi ya Pius Buswita katika harakati za kuokoa.
    Mbao walibadilisha mfumo wa uchezaji baada ya bao hilo na kuanza kucheza kwa kujihami, jambo ambalo liliwasumbua Yanga.
    Kipindi cha pili, Mbao walifanikiwa kuendekea kuwabana Yanga na kujilinda vyema hatimaye kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza ya Mwanza na ya nje ya Dar es Salaam kwa ujumla kufika fainali ya Kombe la TFF.
    Na sasa Mbao FC watakutana na Simba SC katika fainali ya michuano hiyo baadaye mwezi huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Simba iliwatoa washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam FC kwa 1-0 jana, bao pekee la Mohammed Ibrahim.
    Kikosi cha Mbao FC kilikuwa; Benedict Haule, David Mkwasa, Alex Ntiri, Boniface Maganga, Salmin Hoza, Yussuf Ndikumana, Jamal Mwambeleko, George Sangija, Everigustus Bernard/ Robert Ndaki dk73, Pius Buswita na Ibrahim Njohole.
    Yanga SC; Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy/Juma Abdul dk67, Mwinyi Mngwali, Andrew Vicent ‘Dante’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Juma ‘Makapu’/Geoffrey Mwashiuya dk46, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa/Emmanuel Martin dk83, Amissi Tambwe na Haruna Niyonzima.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBAO WAIFUATA SIMBA FAINALI KOMBE LA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top