• HABARI MPYA

    Sunday, April 23, 2017

    SIMBA NA AZAM NUSU FAINALI KOMBE LA TFF, YANGA NA MBAO

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    YANGA SC itamenyana na Mbao FC katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC), Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, lakini Nusu Fainali kali zaidi inatarajiwa kuwa kati ya Azam FC na Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Nusu Fainali ya kwanza itapigwa Aprili 29, Uwanja wa Taifa Jijini na ya pili Aprili 30, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    Hiyo inafuatia droo iliyopangwa leo studio za Azam TV, wadhamini wa michuano hiyo, Tabata mjini Dar es Salaam.
    Ikumbukwe Yanga jana ilikamilisha idadi ya timu za Nusu Fainali za mwaka huu kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa.
    Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Hans Mabena aliyesaidiwa na Mohamed Mkono wote wa Tanga na Arnold Bugado wa Singida, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0 ambayo yote yamefungwa na wachezaji wa kigeni.
    Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Tambwe aliifungia Yanga bao la kwanza dakika 15 kwa kichwa akiunganisha kona ya winga Geoffrey Mwashiuya kutoka upande wa kulia.
    Kiungo mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa naye akawainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 40 akifunga kwa kichwa pia kuunganisha krosi ya beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali.
    Pamoja na Yanga kumaliza dakika 45 za kwanza wakiongoza 2-0, lakini wapinzani wao nao walionyesha upinzani. 
    Mshambuliaji hatari wa Prisons, Jeremiah Juma Mgunda alipiga pembeni dakika ya sita baada ya kufanikiwa kumpita beki wa Yanga, Kevin Patrick Yondani aliyeteleza na kudondoka chini.
    Benjamin Asukile naye akapoteza nafasi ya wazi dakika ya nane baada ya kupiga nje pia kufuatia krosi ya beki Salum Kimenya.
    Kipindi cha pili, Yanga walikianza kwa mabadiliko, kipa wa tatu Benno Kakolanya aliyeanzishwa leo akitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na kipa wa kwanza, Deo Munishi ‘Dida’. 
    Na mwanzoni tu mwa kipindi hicho, winga Simon Happygod Msuva akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 46 kwa shuti kali.
    Dida akaokoa mkwaju wa penalti wa Victor Hangai dakika ya 55 uliotolewa baada ya Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kumchezea rafu Meshack Suleiman.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA AZAM NUSU FAINALI KOMBE LA TFF, YANGA NA MBAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top