• HABARI MPYA

    Tuesday, April 25, 2017

    SIMBA WAINGIA KAMBINI MORO KUJIWEKA SAWA NA AZAM

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Simba kimeingia kambini leo mjini Morogoro kujiandaa na mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) dhidi ya Azam FC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Beki mkongwe, Mzimbabwe Method Mwanjali aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu ni miongoni mwa wachezaji walioingia kambini leo Morogoro, wakati beki mwingine Hamad Juma na kiungo Jamal Mnyate wamebaki Dar es Salaam kwa sababu ya majeruhi.
    Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog amebeba kikosi chake kamili kwa ajili ya vita ya kusaka fainali ya Kombe la ASFC katika kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
    Kwa kufahamu ugumu wa mchezo huo, Simba imekiondoa kikosi chake mjini na kukipeleka Morogoro ili kuelekeza vyema akili zao kwenye mechi hiyo.
    Ikumbukwe Simba wamefungwa na Azam 1-0 mara mbili mfululizo mwezi Janauri, kwanza tarehe 13 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi bao pekee la Himid Mao dakika ya 12 Uwanja wa Amaan, Zanzibar na baadaye tarehe 28 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara bao pekee la Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Na hiyo ilifuatia Simba kuifunga Azam FC 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa kwanza Uwanja wa Taifa, bao pekee la winga Shiza Ramadhani Kichuya dakika ya 67.
    Maana yake Jumamosi itakuwa inawania kuweka rekodi ya kufungana sawa kwa msimu huu na Azam FC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WAINGIA KAMBINI MORO KUJIWEKA SAWA NA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top