• HABARI MPYA

    Saturday, April 29, 2017

    SIMBA WATINGA FAINALI KOMBE LA TFF, SASA WANAISUBIRI YANGA INAMENYANA NA MBAO KESHO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imefanikiwa kwenda Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linalojulikana kama Azam Sports federation Cup baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Sifa zimuendee mfungaji wa bao hilo pekee dakika ya 48, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim ambaye hata hivyo hakumaliza mchezo baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu baadaye.
    Kwa ushindi huo, Simba itasubiri kukutana na mshindi kati ya wenyeji Mbao FC na Yanga SC zinazomenyaa kesho Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mathew Akrama wa Mwanza, Azam FC ilipata pigo dakika ya 15 baada ya kiungo wake mchezeshaji, Salum Abunakar ‘Sure Boy’ kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Hajib.
    Mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Hajib akipasua katikati ya mabeki wa Azam, Shomary Kapombe (kulia) na Aggrey Morris (kushoto)
    Muzamil Yassin (katikati) akipambana na wachezaji wa Azam, Mghana Daniel Amoah (kulia) na Mcameroon Stephan Kingue (kushoto)
    Mshambuliaji wa Azam, John Bocco akimiliki mpira mbele ya mabeki wa Simba
    Winga wa Simba, Shiza Kichuya akimtoka winga wa Azam, Ramadhani Singano 'Messi'
    Kiungo wa Azam, Salum Abubakar akitoka nje baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu leo

    Ilionekana kama wachezaji hao wamegongana kwa kawaida mno, lakini kwa namna Hajib alivyojirusha huku akipiga yowe la kuugulia maumivu Akrama aliingia kwenye mtego wa kumtoa kwa kadi nyekundu Sure Boy.
    Tukio hilo lilileta kizaazaa kidogo uwanjani baada ya wachezaji wa Azam kumfuata refa na kuanza kumlalamikia kwa maamuzi yake. Walinzi wa Uwanja wa Taifa walimfuata Sure Boy na kujaribu kumtoa kwa nguvu, jambo ambalo liliwafanya wavutane na Meneja wa Azam, Philipo Alando.
    Mchezo uliendelea baada ya tukio hilo, huku timu zikiendelea kushambuliana kwa zamu na kabla ya Akrama kupuliza kipyenga cha kumaliza ngwe ya kwanza kukiwa hakuna bao.
    Kipindi cha pili, Simba walikianza vizuri na kufanikiwa kupata bao baada ya dakika tatu tu, kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim akimtungua vizuri kipa Aishi Salum Manula kwa shuti la mguu wa kulia kufuatia ya krosi ya mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo.
    Simba wakaanza kucheza kwa tahadhari kwa kujihami zaidi baada ya bao hilo, huku Azam FC wakionekana kusaka bao la kusawazisha kwa nguvu zao zote.
    Mo Ibrahim akaonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 77 baada ya kumchezea rafu beki wa Azam FC, Shomary Kapombe.
    Beki Mkongo, Janvier Besala Bokungu akaizuia Azam FC kusawazisha baada ya kuokoa mpira uliopigwa kwa kichwa na Nahodha wa timu hiyo, John Raphael Bocco uliokuwa unaelekea nyavuni dakika ya 84.
    Kikosi cha Simba kilikuwa; Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, James Kotei/Said Ndemla dk88, Jonas Mkude, Shizza Kichuya, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo/Mwinyi Kazimoto dk86, Ibrahim Hajib na Mohammed Ibrahim.
    Azam FC; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Aggrey Morris, Daniel Amoah, Himid Mao, Stephan Kingue/Joseph Mahundi dk58, Shaaban Iddi/Frank Domayo dk46, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Ramadhani Singano ‘Messi’/Mudathir Yahya dk82. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WATINGA FAINALI KOMBE LA TFF, SASA WANAISUBIRI YANGA INAMENYANA NA MBAO KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top