• HABARI MPYA

    Sunday, April 23, 2017

    HAJJI MANARA AFUNGIWA MWAKA MMOJA NA FAINI MILIONI 9

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemfungia Hajji Manara, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba kwa mwaka mmoja kutojihusisha na masuala ya soka pamoja na kumpiga faini ya Sh. Milioni 9.
    Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Wakili Jerome Msemwa amewaambia Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya Manara kukutwa na makosa matatu dhidi ya TFF waliomlalamikia.
    Msemwa ameyataja makosa hayo ya Manara dhidi ya mlalamikaji, TFF ni kuituhumu na kuidhalilisha TFF, kueneza chuki za ukabila na la tatu kuingilia utendaji wa shirikisho hilo.
    Kwa makosa hayo yote, anakumbana na adhabu ya kuwa nje ya masuala ya soka kwa mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh. Milioni 9 kabla ya kumaliza adhabu yake.
    Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Wakili Jerome Msemwa akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam   

    Kosa la kwanza amehukumiwa kwa mujibu wa kanuni ya 41 kifungu cha tisa ambalo analipa faini ya Sh. Milioni 1, la pili amehukumiwa kwa kanuni ya 53 kifungu cha kwanza na cha pili na anafungiwa miezi mitatu na faini ya Sh. Milioni 3 na kosa la tatu amehukumiwa kwa kanuni ya kwanza na ya pili inayohusu Maadili, ambayo alitakiwa afungiwe miaka saba na faini ya Sh. Milioni 5.
    Lakini kutokana na kuwa hilo ni kosa lake la kwanza Kamati imetumia mamlaka yake kwa kumpunguzia adhabu hadi miezi 12 na faini ya Sh. Milioni 5 – na adhabu hizo zimeunganishwa, hivyo atatumikia kifungo cha mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh. Milioni 9.
    Hata hivyo, Msemwa alisema Manara hakutokea kwenye kikao cha kutoa utetezi wake dhidi ya tuhuma hizo, ingawa taarifa ya kuitwa alifikishiwa yeye na klabu yake pia. 
    Adhabu hii inafuatia Manara ‘kuishambulia’ TFF    
    Katikati ya wiki, akiituhumu kufanya njama za waziwazi ili kuwabeba wapinzani wao, Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Manara pia aliwatuhumu viongozi wakuu wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa ni wahaya na viongozi wa zamani wa Yanga, ambao wanataka kuipendelea Kagera Sugar na timu yao hiyo ya zamani.
    Na hamaki ya Manara, ilifuatia TFF kulipeleka Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji suala la Simba kupewa ushindi wa mezani na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72.
    Kamati ya Saa 72 iliipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu baada ya kujiridhisha beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi aliichezea timu hiyo dhidi Wekundu wa Msimbazi Aprili 2, mwaka huu akiwa ana kadi tatu za njano, ambayo ni kinyume cha kanuni.
    Lakini siku mbili baadaye, Kagera Sugar wakapinga maamuzi hayo na kuomba suala hilo lisikilizwe upya kwa kuwa mchezaji wao hakuwa na kadi tatu za njano siku wanaifunga Simba 2-0 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAJJI MANARA AFUNGIWA MWAKA MMOJA NA FAINI MILIONI 9 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top