• HABARI MPYA

    Sunday, September 11, 2016

    YANGA WAPO KATIKA MSIMU MGUMU

    BAADA ya michuano ya Euro 2016 Ufaransa, wachezaji kadhaa wakubwa hawakwenda kwenye kambi za maandalizi ya msimu mpya ya klabu zao Julai.
    Walipewa mapumziko kwa sababu waliingia kwenye Euro 2016 wakitokea kwenye Ligi Kuu zao na michuano ya klabu Ulaya.
    Cristiano Ronaldo jana amecheza mechi ya kwanza ya msimu Real Madrid, kwa sababu ni miongoni mwa wachezaji waliopewa mapumziko na klabu zao baada ya Euro.
    Kiungo mpya wa Manchester United, Paul Pogba alichelewa kujiunga na Mashetani hao Wekundu tu kwa sababu ya mapumziko yake Marekani baada ya Euro.
    Klabu zinalazimika kuwapa wachezaji fulani mapumziko baada ya kucheza kwa muda mrefu mfululizo – ili miili yao ipate ahueni kidogo.
    Na hiyo ni kwa sababu tu zinajiendesha kitaalamu, mambo hayaendi kienyeji tofauti na hapa kwetu nchini.
    Tazama Yanga SC wanaonekana kuingia katika msimu mgumu mno wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzani Bara, kutokana tu na wachezaji wake kuchoka baada ya kucheza misimu miwili mfululizo.
    Yanga walianza Ligi Kuu Agosti mwaka jana na Juni mwaka huu wakafanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Msimu wa mashindano ya ndani nchini ulikamilika Mei 25, mwaka huu Yanga wakitwaa mataji yetu matatu, Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
    Baada ya hapo wakaingia kwenye mechi za makundi za Kombe la Shirikisho, ambazo kabla hawajazimaliza tayari wakawa wamekwisharejea kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu.
    Walianza na mechi ya Ngao ya Jamii ambayo walifungwa na Azam FC kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2 na mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu ukaahirishwa ili wacheze mechi ya mwisho ya Kundi A Kombe la Shirikisho dhidi ya TP Mazembe.
    Na ilipofikia, wachezaji wa Yanga, ukiondoa wale wapya kama Juma Mahadhi, Andrew Vincent na Hassan Kessy au waliokuwa majeruhi wakati wa Kombe la Shirikisho kama Deus Kaseke wanaonekana kabisa wamechoka.
    Thabani Kamusoko tunayemuona katika mechi za Ligi Kuu msimu huu si yule wa msimu uliopita hata Mzimbabwe mwenzake, mshambuliaji Donald Ngoma naye pia naye anaonekana kabisa kuchoka.
    Na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm anazidi kuwachosha wachezaji hao kwa kuendelea kuwatumia, tena kwa muda mrefu uwanjani.
    Na inawezekana anaendelea kuwatumia kwa sababu hana wachezaji mbadala baada ya kumuacha Salum Telela na Haruna Niyonzima akiwa majeruhi lazima Kamusoko acheze kila mechi.
    Na wanapokuwa wanacheza Ngoma na Mrundi, Amissi Tambwe mshambuliaji mwingine tunayemuona benchi ni Matheo Anthony pekee baada ya kuachwa kwa Paul Nonga na kwa Malimi Busungu akiwa majeruhi.
    Na bahati mbaya Ratiba ya Ligi Kuu nayo imekaa vibaya kwao, kwani mechi ya kwanza walicheza Dar es Salaam wakashinda 3-0 dhidi ya African Lyon, ya pili wakaenda kutoa sare ya 0-0 na Ndanda mjini Mtwara kabla ya jana kurejea Dar es Salaam 3-0 dhidi ya Maji Maji.
    Sasa Yanga wanakwenda Shinyanga kucheza mechi zote mbili dhidi ya Stand United na Mwadui FC ndani ya wiki moja.
    Yaani unaweza kuona kabisa ambavyo Yanga ipo katika msimu huu mgumu wa 2016-2017, tu kwa sababu wachezaji wake hawajapata muda wa kupumzika tangu msimu uliopita
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAPO KATIKA MSIMU MGUMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top