• HABARI MPYA

    Thursday, August 04, 2016

    TAKUKURU WAPEKUA OFISI YA AVEVA, WAMUACHIA KWA DHAMANA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Simba SC, Evans Elieza Aveva ameachiwa huru baada ya kushikiliwa na Polisi tangu jana jioni kwa tuhuma za kuhamishia fedha za klabu katika akaunti yake binafsi.
    Aveva amehojiwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) leo juu ya kuhamisha zaidi ya dola za Kimarekani 300,000 kutoka akaunti ya klabu kwenda akaunti yake binafsi.
    Fedha ambazo Aveva anadaiwa kuhamisha ni zilizolipwa na Etoile du Sahel ya Tunisia, dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh. Milioni 600 za Tanzania.
    Awali, Etoile walikuwa wazito kulipa fedha hizo kwa sababu walidumu na Okwi kwa miezi sita kabla ya kushindwana na kushitakiana hadi FIFA.
    Aveva ameachiwa kwa dhamana leo baada ya kushikiliwa na Polisi tangu jana

    Etoile ilimtuhumu Okwi kuchelewa kurejea klabuni baada ya kuruhusiwa kwenda kuchezea timu yake ya taifa, wakati mchezaji akadai kutolipwa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu. 
    Mwishowe Okwi aliruhusiwa na FIFA kutafuta klabu ya kuchezea wakati kesi yake na Etoile inaendelea – naye akarejea klabu yake ya zamani, SC Villa ya Uganda, ambayo baadaye ilimuuza Yanga SC mwaka 2014.
    Baada ya nusu msimu, Okwi akavurugana pia na Yanga hadi kufikishana TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ambako aliruhusiwa kuondoka bure Jangwani, hivyo kujiunga tena na Simba SC kama mchezaji huru.
    Simba SC ikamuuza tena Okwi kwa dola za Kimarekani 100,000 klabu ya SonderjyskE ya Ligi Kuu ya Denmark, ambako anakoendelea na kazi hadi sasa. 
    Desemba mwaka jana, FIFA iliipa Etoile siku 60 kuwa imekwishalipa dola 300,000 za Simba SC, vinginevyo watachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufungiwa kucheza mashindano yoyote. 
    Na leo Mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Sekta ya Uma ya TAKUKURU, Leonard Mtalai amesema baada ya fedha hizo kuhamishiwa kwenye akaunti ya Aveva, dola 62,000 zilitumwa Hong Kong, China.
    Mtalai amesema kwa sasa TAKUKURU inashirikiana na Taasisi ya Rushwa ya China kuchunguza ili kujua fedha zilizotumwa Hong Kong zilitumikaje.
    Pamoja na Aveva, Wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC walihojiwa leo na TAKUKURU.
    Na inadaiwa Maofisa wa TAKUKURU walikwenda kufanya ukaguzi ofisini kwa Aveva pia.
    Pamoja na kuachiwa kwa dhamana, Aveva ataendelea kuhojiwa kesho na iwapo atakutwa na hatia atapandishwa mahakamani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAKUKURU WAPEKUA OFISI YA AVEVA, WAMUACHIA KWA DHAMANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top