• HABARI MPYA

    Thursday, August 04, 2016

    AVEVA AWEKWA ‘LUPANGO’ AKIDAIWA ‘KUTOA’ FEDHA ZA OKWI KWENYE AKAUNTI YA SIMBA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Simba SC, Evans Elieza Aveva anashikiliwa na Jeshi la Polisi tangu jana, kufuatia tuhuma za kuhamisha fedha za mauzo ya mshambuliaji Emmanuel Okwi kutoka kwenye akaunti ya klabu.
    Habari ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imezipata zimesema kwamba, Aveva alikamatwa jana jioni na juhudi za kumpatia dhamana hazikuweza kufanikiwa hadi leo.
    Inaelezwa suala lake lipo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambayo bado inaendelea na uchunguzi na ndiyo maana imekuwa vigumu kupatiwa dhamana.
    Aveva (kushoto) akiwa na mfanyabiashara, Mohamed Dewji
    Alipotafutwa Katibu wa Simba SC, Patrick Kahemele kuzungumzia habari hizo, hakuwa tayaeri kusema chochote; “Hili suala mimi siwezi kulizungumzia,”alisema.
    Fedha ambazo Aveva anadaiwa kuhamisha ni zilizolipwa na Etoile du Sahel ya Tunisia, dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh. Milioni 600 za Tanzania.
    Awali, Etoile walikuwa wazito kulipa fedha hizo kwa sababu walidumu na Okwi kwa miezi sita kabla ya kushindwana na kushitakiana hadi FIFA.
    Etoile ilimtuhumu Okwi kuchelewa kurejea klabuni baada ya kuruhusiwa kwenda kuchezea timu yake ya taifa, wakati mchezaji akadai kutolipwa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu. 
    Mwishowe Okwi aliruhusiwa na FIFA kutafuta klabu ya kuchezea wakati kesi yake na Etoile inaendelea – naye akarejea klabu yake ya zamani, SC Villa ya Uganda, ambayo baadaye ilimuuza Yanga SC mwaka 2014.
    Baada ya nusu msimu, Okwi akavurugana pia na Yanga hadi kufikishana TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ambako aliruhusiwa kuondoka bure Jangwani, hivyo kujiunga tena na Simba SC kama mchezaji huru.
    Simba SC ikamuuza tena Okwi kwa dola za Kimarekani 100,000 klabu ya SonderjyskE ya Ligi Kuu ya Denmark, ambako anakoendelea na kazi hadi sasa. 
    Desemba mwaka jana, FIFA iliipa Etoile siku 60 kuwa imekwishalipa dola 300,000 za Simba SC, vinginevyo watachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufungiwa kucheza mashindano yoyote. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AVEVA AWEKWA ‘LUPANGO’ AKIDAIWA ‘KUTOA’ FEDHA ZA OKWI KWENYE AKAUNTI YA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top