• HABARI MPYA

  Wednesday, May 11, 2016

  YANGA KWENDA ANGOLA JUMAPILI, MALINZI AWATUMIA SALAMU ZA PONGEZI

  Na Waandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC itaondoka Dar es Salaam Alfajiri ya Jumapili kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kuingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Sagrada Esperanca katikati ya wiki ijayo.
  Yanga itaondoka Dar es Salaam siku moja tu baada ya kukabidhiwa Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika mchezo dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Taifa.
  Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imeidhinisha mchezo Ndanda na Yanga kuchezwa Uwanja wa Taifa, badala ya Nangwanda Sijaona, Mtwara baada ya klabu hizo kukubaliana.

  Taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas Mapunda imesema kwamba wenyeji wa mchezo huo, Ndanda wamekubali kucheza nyumbani kwa wapinzani wao,Yanga.
  "Kwa wakati tofauti, mwishoni mwa wiki iliyopita Yanga ilituma maombi kwa Ndanda kadhalika TPLB kuomba ridhaa ya mchezo huo kufanyika Dar es Salaam kwa kuwa inatarajiwa kusafiri Jumapili alfajili kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidi ya Sagrada Esperanca," imesema taarifa hiyo..
  Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro ameishukuru Ndanda kwa uungwana wao wa kujali maslahi ya taifa na kukubali mchezo huo kufanyika Dar es Salaam, kabla ya Yanga kwenda Angola.
  Kanuni ya pili ya Ligi Kuu Bara toleo la 2015/16 imeeleza wazi kuwa, “Katika mazingira maalumu, timu inaweza kucheza mchezo wake wa nyumbani katika uwanja mwingine endapo kuna sababu nzito na za msingi, utambulisho wa uwanja katika mazingira haya pia unawajibika kufanywa katika kipindi cha uthibitisho wa kushiriki ligi au kwa maombi maalumu kwa TPLB,” inasehemu kanuni hiyo.
  Kwa kuzingatia kanuni hiyo na sababu za yanga ambazo Ndanda na Bodi wameona kuwa ni nzito wamekubaliana kucheza mchezo huo Dar es Salaam.
  Yanga inatarajiwa kucheza na wapinzani wao, Sagrada Esperanca ya Angola ama Mei 17 au 18, 2016. Katika mchezo wa kwanza ulifanyika Dar es Salaam Jumamosi iliyopita Yanga iliwafunga wageni wake mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Yanga inahitaji ama sare, ushindi na kama kufungwa basi si zaidi ya bao moja ili kuindoa Esperanca katika hatua ya awali, ili kuingia hatua ya makundi katika kusonga mbele.
  Wakati huo huo: Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi ameipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.
  Hii ni mara ya 26 kwa Yanga kutwaa taji tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965, ikifuatiwa na Simba iiliyotwaa mara 18 na Mtibwa Sugar ya Morogoro mara mbili.
  Yanga imefikia rekodi hiyo baada ya kutwaa ubingwa katika miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992,1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006 na misimu ya 2007-2008, 2008-2009, 2010-2011, 2012-2013, 2014-15 na 2015-16.
  “Nichukue nafasi hii kuipongeza Young Africans kwa ubingwa. Pia nizipongeze timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya msimu wa Ligi Kuu Bara ya Vodacom 2015/16 kuwa wenye mafanikio,” amesema Rais Malinzi baada ya Yanga kufikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo.
  Malinzi pia amezikumbusha na kuhamamisha klabu zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2016/17 kutoa maoni, mapendekezo, marekebisho ya ili kuboresha kanuni za uendeshaji wa ligi hiyo kwa msimu ujao. Maoni hayo yapelekwe kwa njia ya maandishi moja kwa moja kwenye ofisi za Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) au kwa njia ya barua pepe tplb.tplb@yahoo.com
  Yanga imetwaa ubingwa huo ikiwa na mechi mbili mkononi, dhidi ya Ndanda Jumamosi na Majimaji Mei 22 Uwanja wa Majimaji, Songea.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KWENDA ANGOLA JUMAPILI, MALINZI AWATUMIA SALAMU ZA PONGEZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top