• HABARI MPYA

    Wednesday, May 11, 2016

    MAYANJA ‘AWAFUNGIA VIOO’ WAGENI SIMBA NA MAJIMAJI, APANGA WATOTO WA NYUMBA WATUPU

    Na Saada Mohamed, SONGEA
    KOCHA Mganda wa Simba SC, Jackson Mayanja (pichani kushoto) amewatupa nje wachezaji wa kigeni katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo dhidi ya wenyeji Majimaji mjini Songea, Ruvuma.
    Mayanja amepanga wazawa watupu kwa ajili ya mchezo huo wa Saa 10:30 Uwanja wa Majimaji, huku katika benchi akimuweka kiungo Mzimbabwe, Justice Majabvi pekee.
    Wachezaji wawili tu, kipa Muivory Coast, Vincent Angban na Majabvi ndiyo wapo Songea kati ya saba waliogoma kusafiri na timu juzi kwa ajili ya mchezo huo.
    Wawili hao waliondoka jana asubuhi, baada ya kikao cha pamoja baina ya wote waliogoma na Rais wa klabu, Evans Aveva kilichofanyika juzi mjini Dar es Salaam.
    Wachezaji hao waligoma kwa sababu ya kucheleweshewa mishahara ya Aprili na uongozi wa Simba ulisema juzi mishahara imechelewa kwa sababu wadhamini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) hawajatoa fedha.
    Habari zisizo za uhakika zinasema Rais Aveva juzi aliwalipa wachezaji hao waliogoma na kuwateua wawili kati yao, Angban na Majabvi kwenda kuiongezea nguvu timu Songea.  
    Wengine waliogoma ni beki Mrundi Emery Nimubona, kiungo mzawa Mwinyi Kazimoto, Waganda beki Juuko Murshid, kiungo Brian Majwegga na mshambuliaji Hamisi Kiiza.
    Mbali na hao waliogoma Simba kesho inawakosa pia viungo Jonas Mkude, Awadhi Juma na washambuliaji Ibrahim Hajib na Raphael Kiongera, ambao nao hawajasafiri na timu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwa majeruhi na kutumikia adhabu za kadi.
    Kikosi alichopanga Mayanja leo ni; Peter Manyika, Said Issa, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Mohammed Fakhi, Hassan Isihaka, Novaty Lufunga, Said Ndemla, Abdi Banda, Mussa Mgosi, Peter Mwalyanzi na Mohammed Mussa.
    Katika benchi wapo kipa David Robert Kissu, Freddy Anthony, Hussein Magila, Said Hamisi na Majabvi. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAYANJA ‘AWAFUNGIA VIOO’ WAGENI SIMBA NA MAJIMAJI, APANGA WATOTO WA NYUMBA WATUPU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top