• HABARI MPYA

  Thursday, May 05, 2016

  WAGHANA KUCHEZESHA YANGA NA WAANGOLA TAIFA JUMAMOSI

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MAREFA wa Ghana watachezesha mechi ya kwanza ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya wenyeji, Yanga dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola.
  Hao ni Joseph Odartei Lamptey atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera David Laryea na Malik Alidu Salifu.
  Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Alfred Lucas Mapunda amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba Kamisaa wa mchezo huo ni Asfaw Luleseged Begashaw kutoka Ethiopia.
  Kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm (kulia) akiwa na Meneja, Hafidh Saleh

  Mwandishi huyo wa zamani wa gazeti la Dimba amesema kwamba waamuzi watawasili leo usiku nchini, wakati Kamisaa atawasili kesho. 
  Mchezo wa marudiano utachezeshwa na marefa wa Madagascar Mei 17, mwaka huu Uwanja wa Sagrada Esperanca, zamani Quintalao do Dundo na utachezweshwa .
  Hao ni Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.
  Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
  Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani. Katika Raundi ya kwanza wakaitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAGHANA KUCHEZESHA YANGA NA WAANGOLA TAIFA JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top