• HABARI MPYA

    Sunday, May 01, 2016

    MAREFA WA MADAGASCAR KUICHEZESHA YANGA ANGOLA

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MAREFA kutoka nchini Madagascar watachezesha mchezo wa marudiano wa mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kati Sagrada Esperanca na Yanga SC ya Tanzania Mei 17, mwaka huu Uwanja wa Sagrada Esperanca, zamani Quintalao do Dundo.
    Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE marefa hao ni Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.
    Yanga itawania kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho

    Hata hivyo, CAF bado haijateua marefa wa kuchezesha mechi ya kwanza baina ya timu hizo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Mei 7. 
    Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
    Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
    Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani. Katika Raundi ya kwanza wakaitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAREFA WA MADAGASCAR KUICHEZESHA YANGA ANGOLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top