• HABARI MPYA

  Saturday, May 07, 2016

  KILA LA HERI YANGA SC, USHINDI WENU NI HESHIMA YETU SOTE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya Afrika, Yanga SC leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Sagrada Esperanca ya Angola.
  Huo ni mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika na timu hizo zitarudiana wiki ijayo Angola. 
  Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa
  wachezaji wake wawili tegemeo wa kimataifa wa Zimbabwe, kiungo Thabani Scara Kamusoko na mshambuliaji Donado Dombo Ngoma, ambao wanatumikia adhabu ya kadi za njano mfululizo walizopewa katika mechi dhidi ya Al Ahly mwezi uliopita.

  Mchezo huo utachezeshwa na marefa kutoka Ghana, ambao ni Joseph Odartei Lamptey atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera David Laryea na Malik Alidu Salifu, wakati Kamisaa ni Asfaw Luleseged Begashaw kutoka Ethiopia.
  Kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm anatarajiwa kuwatumia Haruna Niyonzima katika sehemu ya Thabani Kamusoko na haijulikani kati ya Malimi Busungu na Paul Nonga nani ataziba pengo la Ngoma.
  Kuwakosa Kamusoko na Ngoma, wazi Yanga itakosa vitu fulani muhimu na haitatarajiwi kuwa na makali ya kiwango chake.
  Amissi Tambwe hajaonyesha makali ya kufunga katika mechi ngumu za michuano ya Afrika, hivyo pengo la Ngoma linaweza linamuumiza kichwa hata kocha Pluijm.
  Katika kiungo hakuna shaka sana kukosekana kwa Kamusoko, kwani mbali na Niyonzima kuna Salum Telela, Said Makapu na Mbuyu Twite.
  Viingilio vya mchezo wa leo ni Sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, wakati viti vya bluu na kijani watu wataketi kwa Sh. 7,000, VIP B na C watu wataketi kwa Sh 20,000 na VIP na VIP A  itakuwa Sh.30,000.
  Mchezo wa marudiano utachezeshwa na marefa wa Madagascar Mei 17, mwaka huu Uwanja wa Sagrada Esperanca, zamani Quintalao do Dundo na utachezweshwa .
  Hao ni Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.
  Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
  Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani. Katika Raundi ya kwanza wakaitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
  Kila la heri Yanga SC. Mungu ibariki Yanga, Mungu ibariki Tanzania. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA LA HERI YANGA SC, USHINDI WENU NI HESHIMA YETU SOTE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top