• HABARI MPYA

  Sunday, May 01, 2016

  KAZI IPO TAIFA LEO AZAM NA SIMBA LIGI KUU

  Na Somoe Ng’itu, DAR ES SALAAM
  NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo zinatarajiwa kuwaka moto kwa mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Azam FC na Simba.
  Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 58 na Simba 57 katika nafasi ya tatu, kwa pamoja zinaifukuzia Yanga katika mbio hizo za ubingwa, ambayo ipo kileleni baada ya kufikisha jumla ya pointi 65 kufuatia ushindi wa jana wa 2-1 dhidi ya Toto Africans mjini Mwanza.
  Mabingwa hao wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) imefanya maandalizi ya nguvu kukabiliana na Wekundu hao, ambao wenyewe walienda kujichimbia visiwani Zanzibar kujiandaa na mtanange huo, hivyo mchezo huo unatarajia kuwa na upinzani mkali kwa pande zote mbili.

  Winga Farid Mussa wa Azam FC akitoa pasi mbele ya beki wa Simba SC, Hassan Isihaka kwenye mchezo uliopita timu hizo zikitoka sare ya 2-2

  Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi katika mchezo uliopita dhidi ya Majimaji ya Songea (2-0) mabao yote yakifungwa na kiungo Mudathir Yahya, huku bao pekee lililofungwa na mshambuliaji wa Toto Africans, Wazir Junior, likiizamisha Simba ndani ya Uwanja wa Taifa.
  Azam FC itawakosa wachezaji wengine kama kiungo Frank Domayo, Allan Wanga, Racine Diouf, Shomari Kapombe, ambao ni wagonjwa huku Nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, akiendelea kukosekana kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoipata wakati timu hiyo ikiichapa Mtibwa Sugar bao 1-0.   
  Mchezo wa kwanza baina ya hizo katika mzunguko wa kwanza uliisha kwa sare ya mabao 2-2, Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ akifunga mabao yote, wakati Ibrahim Hajibu alifunga ya Simba mabao.  
  Huo utakuwa mchezo wa 16 kuzikutanisha timu hizo kwenye ligi tangu Azam FC ipande msimu wa 2008/2009, Azam ikishinda nne, Simba saba na kutoka sare mara nne.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAZI IPO TAIFA LEO AZAM NA SIMBA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top