• HABARI MPYA

  Friday, May 20, 2016

  FARID AREJEA DAR, AZAM YAGOMA KUMUUZA ‘BEI CHEE’ HISPANIA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imekataa kumuuzaa Farid Malik Mussa klabu ya Daraja la Kwanza Hispania, Deportivo Tenerife, lakini iko tayari kumtoa kwa mkopo wa makubaliano maalum.
  Farid amerejea leo jioni Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Azam FC, Yussuf Bakhresa aliyekuwa anafuatilia majaribio ya mchezaji huyo Hispania ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba Tenerife wameleta ofa, lakini dau lao ni dogo.
  “Sisi hatutaki kuwanyima huyu mchezaji, nia yetu wamuendeleze ili afike mbali afungue milango ya Watanzania wengine kucheza Hispania ambako ndiko kuna soka bora,”amesema Yussuf Bakhresa na kuongeza; “Lakini ofa yao waliyitoa ni ndogo sana,”.
  Farid Mussa (kushoto) akiwa na bosi wake, Yussuf Bakhresa walipokuwa Hispania

  Yussuf amesema wamewajibu Tenerife wakiwaambia wako tayari kuwapa mchezaji huyo kwa mkopo wa makubaliano maalum, lakini si kumuuza ‘bei karibu na bure’.
  “Ataendelea kuwa mchezaji wa Azam, sisi tutawapa wamtumie kwa mkopo, na ikitokea ofa ya wao kumuuza, tutakaa nao chini tumuuze kwa pamoja,”amesema.   
  Yussuf amesema wakati wanasubiri majibu ya Tenerife na hatima nzima ya suala hilo, Farid ataendelelea na kazi Azam FC. 
  Farid alitua Hispania Aprili 21 baada ya kuichezea Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance mjini Tunis, Tunisia ikifungwa 3-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
  Farid Mussa wakati anawasili leo Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam

  Na ilimchukuwa wiki moja tu Farid kuwakuna kwa kipaji chake makocha wa Tenerife na kuamua wanamnunua.
  Hata hivyo, Farid alibaki Hispania kusubiri makubaliano baina ya Azam FC na Tenerife, lakini baada ya kuanza kuwa magumu amerejea nyumbani.
  Na Farid amerejea nyumbani katika wakati mwafaka, kwani ameitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kitakachocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Kenya mjini Nairobi, Mei 29.
  Kikosi hicho kinatarajiwa kuingia kambini Jumatatu pamoja na maandalizi dhidi ya Harambee Stars, lakini pia kujiandaa kwa mchezo dhidi ya Misri kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: FARID AREJEA DAR, AZAM YAGOMA KUMUUZA ‘BEI CHEE’ HISPANIA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top