• HABARI MPYA

    Friday, May 20, 2016

    MAPOKEZI YA YANGA LEO ‘YALIKUWA OVYO’ KABISA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KUTOANDALIWA kwa utaratibu mzuri wakati wa mapokezi ya Yanga SC leo wakirejea kutoka Angola kumewanyima fursa mamia ya mashabiki waliojitokeza kuilaki timu hiyo kufurahia na mashujaa wao.
    Yanga imerejea leo kutoka Angola ambako juzi iliitoa Sagrada Esparanca katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutinga hatua ya makundi.
    Yanga imesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya kushinda 2-0 wiki iliyopita Dar es Salaam na juzi kufungwa 1-0 mjini Dundo, Angola.
    Na mashabiki wa timu hiyo walimiminika kwa wingi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kuwalaki mashujaa wao, hususan kipa Deo Munishi ‘Dida’ aliyepangua mkwaju wa penalti dakika za lala salama.
    Lakini hata hivyo, kukosekana utaratibu mzuri wa wachezaji kupitishwa mbele ya mashabiki kuanzia wakati wanatoka JNIA hadi wanapita kuelekea kwa Mwenyekiti wao, Quality Centre kuliwanyima raha mashabiki.
    Wachezaji wa Yanga wakipita kwenye basi lao huku mashabiki wakiwa na kiu ya kuwaona mashujaa wao

    Ilitarajiwa Yanga wangeandaa gari kubwa la wazi ambalo wachezaji wangeonekana vizuri kwa mashabiki wao na kuwafurahia zaidi, lakini badala yake walipakizwa kwenye basi na hivyo kutoonekana.
    Kwa kawaida mapokezi ya aina hata Ulaya, wachezaji hutembezwa kwenye basi la wazi kufurahia na mashabiki wao – lakini Yanga leo walifichwa kwenye basi.
    Hata wakati wa kutoka JNIA, wachezaji walitolewa ‘kama mateka’ na kukimbizwa kwenye basi wakiwakwepa mashabiki.
    Ilitarajiwa kungekuwa na utaratibu mzuri tangu mapema kwa kuweka vizuizi baina ya mashabiki na kuacha njia ya wachezaji kupita katikati wakiwapungia mashabiki, lakini haikuwa hivyo.
    Kipa Deo Munishi 'Dida' akikimbizwa kuwahishwa kwenye basi kuwakwepa mashabiki

    Lilikuwa tukio kubwa katika historia ya Yanga na nchi kwa ujumla kisoka, lakini kutokana na kukosekana ubunifu, mashabiki wa timu hiyo hawakupata faraja waliyoitarajia, iliyowafanya wakaacha shughuli zao na kukusanyika JNIA.
    Mwaka 2003 wakati Simba SC inarejea kutoka Misri iliitoa Zamalek na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uliandaliwa utaratibu mzuri wachezaji wakibebwa kwenye gari la wazi hadi Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), ambako ilifanyika tafrija fupi chini ya mgeni rasmi, Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
    Mwaka 2008 timu ya taifa, Taifa Stars iliporejea kutoka Sudan ambako iliwatoa wenyeji na kukata tiketi ya kucheza fainali za kwanza za CHAN 2009 kadhalika wachezaji walipitishwa kwenye gari la wazi.
    Kwa ujumla mashabiki wa Yanga leo wamenyimwa raha waliyoitarajia kutokana na tukio la kihistoria na la kishujaa la timu yao.
    Mashabiki wa Yanga wakining'inia kwenye basi kuwachungulia wachezaji wao
    Walioboreka walirudi kwenye magari yao na kuondoka bila kushiriki maandamano
    Mashabiki wenye moyo zaidi walisindikiza basi barabara ya Nyerere

    Tanzania iliingiza timu kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Afrika mara ya mwisho mwaka 2003, wakati huo Jakaya Mrisho Kikwete bado si rais wa Tanzania hadi akaingia Ikulu 2005 na kumaliza muda wake.
    Mwaka 2003 hata Uwanja wa mpya wa Taifa haujafikiriwa kuanza kujengwa na leo unakaribia muongo mmoja tangu uanze kutumika.  Hata  Leodegar Tenga hajawa rais wa TFF hadi ametumikia awamu tatu na kuondoka.
    Mwaka 2003, Rais wa sasa wa TFF, Jamal Malinzi alikuwa Katibu wa Yanga na Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye alikuwa mwanafunzi wa Chuo cha Diplomasia, Kurasini Dar es Salaam.
    Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) haijaanza kudhamini timu za Simba na Yanga – na kwa ujumla mafanikio haya yanakuja katika mwongo na zama mpya kabisa za digitali, lakini hayakupewa heshima stahili.
    Hakukuwa na kiongozi yeyote wa kitaifa kama ilivyokuwa mwaka 2003 kwa Simba au 2008 kwa Taifa Stars – angalau mwaka 1999 wakati Yanga inarejea kutoka Uganda ambako ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Luteni Mstaafu, Yussuf Makamba aliongoza mapokezi.  
    Hakukuwa hata na kiongozi wa juu wa TFF na zaidi alionekana Ofisa mdogo, Jemedari Said ambaye naye alionekana ‘yupo yupo tu’ JNIA. 
    Kwa ujumla mashabiki na wachezaji wa Yanga hawakutendewa haki leo katika mapokezi ya timu yao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAPOKEZI YA YANGA LEO ‘YALIKUWA OVYO’ KABISA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top