• HABARI MPYA

  Wednesday, May 11, 2016

  AVEVA ANGEKUWA MTU WA KUSHAURIKA, SIMBA ISINGEKUWA VIPANDE

  MARA tu baada ya uchaguzi Mkuu uliopita wa Simba SC Juni mwaka 2014 niliandika kuuambia uongozi mpya wa klabu hiyo umuhimu wa kurejesha umoja ndani ya klabu yao.
  Katika uchaguzi huo uliofanyika bwalo la Maofisa wa Polisi, Oyster Bay, Dar es Salaam, Evans Elieza Aveva alichaguliwa kuwa Rais wa klabu hiyo, wakati Geoffrey Hiriki Nyange ‘Kaburu’ akachaguliwa kuwa Makamu wa Rais.
  Iddi Kajuna, Said Tulliy, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour walichaguliwa kama Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
  Uongozi huo ulichukua nafasi ya uongozi wa Alhaj Ismail Aden Rage uliomaliza muda wake.
  Mchakato wa uchaguzi wa Simba uligubikwa na mgogoro uliogawa klabu pande mbili, upande wa kwanza ambao ndiyo ulikuwa na watu wengi ni ule uliomuunga mkono Aveva na kundi lake la Friends Of Simba, wakati upande mwingine ni uliomuunga mkono mgombea aliyeenguliwa, Michael Richard Wambura.

  Wambura alienguliwa mara mbili, kwanza akidaiwa si mwanachama halali wa klabu hiyo, kwa sababu aliwahi kuipeleka klabu hiyo mahakamani na FIFA inakataza masuala ya soka kupelekwa mahakama za dola.
  Kwa kosa hilo, Wambura akakata rufaa Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambako alishinda na kurejeshwa kwenye mbio.
  Akitaja hukumu yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya TFF, Wakili Julius Lugaziya alisema kwamba amemrejesha Wambura kwa sababau, Simba wenyewe walikwishamrejesha na kumuingiza hadi kwenye Kamati ya Utendeaji.
  Lugaziya alisema, baada ya kosa alilolifanya Wambura kuipeleka klabu mahakamani, lakini aliendelea kuhudhuria mikutano, kulipia ada zake za uanachama hata akateuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji.
  Wambura akafanya kosa lingine, wakati anazungumza namna alivyoyapokea maamuzi ya Kamati ya Rufani, akajikuta anazungumza maneno ambayo mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC yalitafsiriwa kuwa ya kikampeni, wakati muda wa zoezi hilo ulikuwa haujafika.
  Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Dk Damas Daniel Ndumbaro ikamuengua tena Wambura kwa kosa la kufanya kampeni kabla ya muda, hivyo alikiuka kanuni za uchaguzi.
  Wambura alikata tena Rufaa TFF, kwa bahati mbaya kwake, akakwama na kuondolewa moja kwa moja kwenye uchaguzi.
  Wafuasi wake wakafungua kesi mahakama ya dola, wakitaka uchaguzi uzuiwe, lakini kwa kuwa hawakujipanga vizuri na hawakuwa na hoja, wakakwama na uchaguzi ukafanyika Jumapili ya mwisho ya Juni, 2014.
  Pamoja na kundi la Aveva kuibuka washindi baada ya sakata zima hilo, lakini hakukuwa na sababu za wana Simba kuendelea kuwa maadui wao kwa wao.
  Inafahamika Simba SC kama timu, mahasimu wao ni Yanga SC- hao ndiyo wa kushindana nao na kuwekeana chuki labda, ingawa katika soka ya dunia ya leo nayo hiyo si sawa sana.
  Dunia ya leo upinzani wa soka unaishia uwanjani, watu wakikutana kwenye vilinge vingine wanaendelea kufurahia pamoja.
  Ndiyo maana, mtu wa Yanga anaoa wa Simba, na kwa pamoja tunategemeana katika mahitaji mbalimbali. Baba anazaa mtoto ni timu tofauti na yake, lakini hata akijiita Simba au Yanga tofuti na baba yake, lakini atabaki kuwa mtoto wa fulani tu.   
  Hatuna uadui siku hizi kwenye mpira, unakwenda uwanjani, timu yako inafungwa 5-0 unarudi nyumbani taratibu na ukifika wa kwanza wa kukutania mwanao, au mkeo.
  Hiyo maana yake sasa mpira ni furaha na si uadui na ni ushamba mkubwa kuifikisha dhana ya upinzani wa mpira kwenye uadui.
  Hivyo basi, nikawaasa Simba SC kutojiruhusu kuendelea kuwa na matabaka miongoni mwao, kwani kufanya hivyo ni kuharibu taswira ya klabu yao.
  Kila kitu kilichosimama imara lazima kiwe na msingi wake wa ujenzi- nilimshauri Aveva achague kuwae msingi wa kurejea kwa umoja na amani ndani ya klabu hiyo.
  Kweli, Wambura alikosea, lakini nilimuambia Aveva kuendelea kupambana naye na kutaka kumkomoa, au kumuadhibu kwa makosa aliyoyafanya kutakuza uhasama.
  Na hakukuwa na sababu ya kukuza uhasama baina ya wana Simba, ikiwa tunaweza kujiridhisha kwamba michezo ni furaha na si chuki.
  Wambura mbishi, wengi wetu tunamjua. Kuomba radhi ni jambo gumu kwake hata kama kweli naye anajua amekosea, bali ataendelea kupambana tu kwa njia nyingine.
  Na kwa kuwa uchaguzi ulifanyika kwa amani na viongozi wapya wakaptikana, niliwashauri Simba kuzika tofauti zao na kurudisha umoja katika klabu yao.
  Takriban miaka miwili sasa tangu aingie madarakani, Simba haifanyi vizuri na tayari uongozi umekwishaanza kulalamika kuna makundi ya watu yanawatumia wachezaji kuihujumu timu ili viongozi waonekane hawafai.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amekaririwa akisema kuna kundi la watu wasiotakia mema klabu hiyo linawashawishi uovu wachezaji wa klabu hiyo.
  Hans Poppe amesema kwamba kundi hilo linawashawishi wachezaji kucheza chini ya kiwango na kuleta migomo baridi ili kuuchafulia uongozi uliopo madarakani.
  Kauli hiyo ya Poppe ilifuatia baadhi ya wachezaji wa Simba SC kuegoma kwenda Songea juzi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Majimaji leo.  
  Wachezaji saba wa Simba wakiwemo sita wa kigeni, wamegoma kusafiri kwenda Songea mkoani Ruvuma kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Majimaji keshokutwa Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
  Na sita wa kigeni, kipa Vincent Angban (Ivory Coast), mabeki Emery Nimubona (Burundi), Juuko Murshid (Uganda), viungo Justice Majabvi (Zimbabwe), Brian Majwega (Uganda), Hamisi Kiiza (Uganda) wamegoma kusafiri.
  Kiungo mkongwe, Mwinyi Kazimoto ni mchezaji pekee anayetumia hati ya kusafiria ya nyumbani aliyegoma kusafiri na wote ni kwa sababu moja, wamecheleweshewa mishahara ya Aprili.
  “Kuna msukumo unatoka nje ndiyo unafanya hivyo, maana mishahara kila mwezi huwa wanapata tarehe hizi, na hiyo ni kwa sababu wadhamini TBL (Kampuni ya Bia Tanzania) wanachelewa kutoa fedha hizo za mishahara,”alisema Hans Poppe.
  Bahati nzuri juzi kilifanyika kikao baina ya wachezaji hao na Rais Aveva ambaye imedaiwa aliwalipa na kuteua wawili, Angban na Majabvi kwenda kuiongezea timu Songea leo, ambao waliondoka kwa basi asubuhi ya jana.
  Lakini tunarudi kule kule, mambo ni magumu kwa uongozi wa Aveva kwa sasa na tayari wameanza kuhisi juhudi zao zinakwamishwa kwa makusudi na maadui zao. 
  Mimi niliyajua haya na ndiyo maana nikawaasa mapema Simba juu ya umuhimu wa kurejesha umoja ndani ya klabu.
  Waswahili wanasema wakutanapo mafahari wawili, ziumiazo nyasi – basi katika mgogoro huu akina Aveva wakiendelea kupambana na maadui zao, inayoathirika ni Simba kama klabu.
  Umefika wakati Simba wakubali kuwa na mwanzo mpya mzuri, wakazika tofauti zao na tukaletewa picha Aveva akiwa ameshikana mikono na akina Rage, Wambura kututhibitishia Simba sasa Nguvu Moja. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AVEVA ANGEKUWA MTU WA KUSHAURIKA, SIMBA ISINGEKUWA VIPANDE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top