• HABARI MPYA

    Saturday, April 09, 2016

    YANGA YAWAKATALIA WAARABU DAR, SARE 1-1

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa kwanza hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa matokeo, Yanga italazimika kwenda kushinda ugenini ili kutimiza ndoto za kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili katika historia yao baada ya mwaka 1998.
    Katika mchezo wa leo, mabao yote yalipatikana kipindi cha kwanza, Ahly wakitangulia kufunga kupitia kwa mshambuliaji wake mjanja, Amr Gamal, kabla ya Yanga kusawazisha kwa bao la ‘ngekewa’ la Issoufou Boubacar.
    Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma akifumua shuti likiwapita wachezaji wa Al Ahly leo Uwanja wa Taifa
    Issoufou Boubacar akikimbia kushangilia baada ya kuifungia Yanga bao la kusawazisha
    Kipa Sherif Ekramy akiushuhudia mpira ukitinga nyavuni baada ya juhudi za beki wake, Ahmed Hegazzy kuokoa kushindikana
    Kungo wa Yanga, Thabani Kamusoko akimtoka kiungo wa Al Ahly, Hossan Ghaly
    Amr Gamal akiwaongoza wenzake kushangilia baada ya kuifungia Al Ahly bao la kuongoza
    Beki wa Yanga, Juma Abdul akiwapita wachezaji wa Al Ahly
    Gamal alifunga kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Ramadan Sobhi dakika ya 10, ambao uliwapita mabeki wote wa Yanga na kipa wao, Ally Mustafa ‘Barthez’ na kumkuta mfungaji pembeni ya lango akaujaza nyavuni.
    Yanga walitulia baada ya baada ya bao hilo na kuanza kupanga mashambulizi yao vizuri, hatimaye kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 18 kupitia kiungo wa Niger, Boubacar.
    Boubacar aliyeukata vizuri mpira kutoka pembeni kushoto mithili ya krosi lakini ukawapita wachezaji wote na kutinga nyavuni.
    Beki Ahmed Hegazzy alijaribu kunyoosha mguu kuutoa mpira, lakini hakufanikiwa jambo ambalo lilimfanya hata kipa wake, Sherif Ekramy asitishe juhudi za kuokoa akiamini mwenzake atafanikiwa.
    Baada ya bao hilo, Yanga waliuteka mchezo na kushambulia mfululizo langoni mwa Ahly, lakini wakaishia kunyooshewa vibendera vya kuotea na msaidizi namba moja wa refa, Marius Donatien.
    Kwa ujumla marefa wa leo kutoka Ivory Coast wakiongozwa na Denis Dembele na Moussa Bayere mshika kibendera wa pili, walionekana kuwasaidia Ahly.
    Kipindi cha pili, Al Ahly walionekana kucheza kwa kujihami zaidi kana kwamba wanataka mchezo umalizike kwa sare – jambo ambalo walifanikiwa.
    Pamoja na matatizo ya marefa, wachezaji wengi wa Yanga nao hawakuwa makini na wenye kujiamini sana, ukiondoa Juma Abdul, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko na Ngoma.
    Na kipindi cha kwanza Yanga walizidiwa kwenye eneo la kiungo kutokana na kutumia watu wawili katikati, Salum Telela na Kamusoko, wakati Al Ahly walikuwa wana watu watatu.
    Kidogo Yanga walianza kucheza vyema kipindi cha pili, baada ya kuingia kwa Simon Msuva na Godfrey Mwashiuya kuchukua nafasi za Boubacar na Amissi Tambwe, ambaye leo mchezo ulimshinda kabisa.
    Deus Kaseke alikwenda kuongeza nguvu katika safu ya kiungo na hapo angalau Yanga ikanza kuonekana inacheza – hata hivyo bahati haikuwa yao.
    Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Aprili 19 mjini Cairo na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi, wakati timu itakayotolewa itaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi kombe la Shirikisho.
    Kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’/Deo Munishi ‘Dida’ dk81, Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Deus Kaseke, Salum Telela, Amissi Tambwe/Simon Msuva, Donald Ngoma, Issoufou Boubakar/Godfrey Mwashiuya dk62.
    Al Ahly. Sherif Ekramy, Mohamed Hany, Sabry Raheel, Rami Rabea, Ahmed Hegazy, Ahmed Fathi, Abdallah Said, Hossam Ghally/Hossan Ahour dk73, Amri Gamal, Ramadan Sobhi/ Waridi Suleyman dk68 na Moaem Zakaria/Malick Evouma dk85.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAWAKATALIA WAARABU DAR, SARE 1-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top