• HABARI MPYA

    Monday, April 25, 2016

    AYA 15 ZA SAID MDOE: NISEMEJE BMM BAND, UGUA POLE AU REST IN PEACE?

    Awali ya yote nichukue fursa hii kusema kuwa bendi ya BMM imesimamisha maonyesho yake kwa muda usiojulika na itakapoibuka itakuwa na sura mpya mpya na pengine hata jina jipya.
    Hii si mara ya kwanza kwa BMM Band kusimamisha maonyesho yake na kuanza upya, ilishafanya hivyo katika utawala wa mwimbaji chipukizi wa dansi Shazzy Sharey, ikafanya hivyo tena kipindi cha uongozi wa Athanas Montanabe.

    Kwa kifupi BMM si bendi mpya kama ambavyo wengi wamekuwa wakifikiria, ni bendi ambayo ilikuwepo hata kabla ya ujio wa Mule mule na Totoo ze Bingwa huku maskani yake ya kudumu yakiwa pale BMM Pub iliyoko Sinza jirani na Mamlaka ya Mapato (TRA) ambapo ilikuwa na kawaida ya kipiga kila siku za wikiendi kwa kiingilio maarufu cha “kinwaji chako”.
    Labda tu, watu watu waliamini kuwa ni bendi mpya baada ya kusukwa upya kwa muungano wake na kundi la Ngwasuma de Bonavida ya Totoo ze Bingwa na Mule Mule na kusajiliwa upya BASATA na kisha kuandaliwa onyesho maalum la utambulisho wa bendi pale Mzalendo Pub.
    Lakini sio Totoo na Mule Mule tu, bali pia BMM sasa ikawa na bodi ya wakurugenzi ambao kwa pamoja walitambulishwa siku ya uzinduzi wa bendi na kutoa picha kuwa upo uwekezaji mkubwa umewekwa ndani ya bendi hiyo.
    Naomba nikiri kuwa kwa bahati mbaya sana, mimi nilikuwa mtabiri wa kimya kimya juu ya uhai wa bendi hiyo – niliamini kuwa haitafika mbali kabla haijakaa tena chini.
    Ile bodi ya wakurugenzi iliyotambulishwa pale Mzelendo Pub ilinitisha, nilikuwa nimeketi sambamba na mkurugenzi wa Aset inayomiliki Twanga Pepeta, mamaa Asha Baraka na nikamwambia kuwa hapa hakuna uhai wa bendi, akanishangaa tu.
    Kwanini bodi ile ya wakurugenzi ilinitisha? Ilinitisha kwasababu sikuona miongoni mwao sura ya muziki bali niliona sura ya wafanya biashara, sura ya watafutaji ambao hawatakuwa na subira ya kungoja mwaka mzima au zaidi ili kuanza kuonja japo senti tano ya faida ya uwekezaji wao.
    Kuwekeza kwenye muziki hapa Bongo si jambo la mchezo, soko ni finyu, kinachongia ni kidogo kuliko unachotoa na kama huna mahaba na muziki, huwezi kufika hata mwezi mmoja kabla hujagundua kuwa umeingia kwenye biashara ‘kichaa’.
    Biashara ya muziki Bongo haitaki kufuata mkumbo, usiingie tu kwa sababu fulani yupo bali zama na ufanye utafiti wa kutosha, wako watu wanadumu kwenye biashara ya muziki kwa sababu tu muziki upo kwenye damu, kwasababu tu wana wadau wanaochangia maendeleo ya bendi, kwasababu tu wanaridhika na kile kidogo wanachovuna.
    Ukiingia kwenye muziki (hususan huu wa bendi za dansi na taarab) kwa misingi ya kuja kuvuna mamilioni, utajikuta uko nje ya ‘game’ bila kujua ni mlango gani uliotokea.
    Kwa bahati mbaya nyingine, ni kwamba sikuwahi kushuhudia onyesho lingine la BMM Band iliyosukwa upya zaidi ya lile la uzinduzi, nilikuwa kila nikiifikiria kwenda napatwa na huzuni, sikuwa na raha ya kwenda kuiona, sikupenda kwenda kuwaangalia maswahiba zangu Totoo ze Bingwa na Mule Mule katika eneo ambalo halikuwa muafaka kwao.
    Naamini sana katika ubora wao Totoo ze Bingwa na Mule Mule, sikuwahi kuigundua dosari yoyote kwao (ya kimuziki) tangu niwafahamu na hata onyesho lao la Mzalendo Pub lilikuwa zuri sana lakini aina ya wamiliki wao ilikuwa ni tatizo.
    Hivi kweli unakwenda kuizindua bendi huku una wimbo mmoja mkononi ambao hauna promosheni ya kutosha na wala hauna video halafu unategemea bendi isimame? Unafanya maonyesho mengine bila matangazo ya radio, posters wala P.A, hakuna fitna magezitini wala mitandaoni halafu unategemea watu waje ukumbini?
    Nimeongea na Totoo ameniambia kuwa bendi imesimama kwa muda wa mwezi mmoja na kwamba wataibuka upya kivyaovyao (yeye na Mule Mule) lakini kwa ufadhili wa vyombo kutoka kwa hao hao wamiliki wa BMM Band. Nawatakia kila kheri, mchango wao ni mkubwa na unahitajika, ila kwasasa bado sielewi, sijui niseme ugua pole au rest in peace BMM Band! Ni jambo la kusubiri.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: NISEMEJE BMM BAND, UGUA POLE AU REST IN PEACE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top