• HABARI MPYA

    Sunday, April 24, 2016

    VURUGU ZAVUNJA MECHI YA COASTAL NA YANGA, REFA AJERUHIWA KWA MAWE MKWAKWANI

    Na Mahmoud Zubeiry, TANGA
    MCHEZO wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup kati ya wenyeji, Coastal Union na Yanga na Dar e Salaam umevunjika baada ya dakika 110.
    Mchezo huo ulivunjika wakati Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-1 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kufuatia mshika kibendera namba mbili kupasuliwa juu ya jicho la kushoto kwa jiwe lililotupwa na shabiki.
    Coastal Union ilitangulia kwa bao la kiungo Mcameroon, Youssouf Sabo kabla ya Yanga kusawaziha kupitia kwa mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma, mabao yote kipindi cha pili.
    Kiungo wa Yanga, Deus Kaseke akimuacha chini beki wa Coastal Union, Adeyoum Ahmed

    Mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe akaifungia Yanga bao la pili mwanzoni tu mwa dakika 30 za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.
    Coastal Union ilimaliza pungufu baada ya beki wake, Adeyoum Saleh Ahmed kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 103 kwa kosa la kushika mpira kwa makusudi.
    Sabo aliiifungia Coastal Union bao la kwanza dakika ya 54 akiunganisha krosi ya Ayoub Yahaya, kabla ya Ngoma kusawazisha Yanga dakika ya 60 akimalizia krosi ya winga Simon Msuva baada ya mabeki wa Coastal Union kusimama wakidhani ameotea.
    Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, Coastal Union ndiyo waliotawala zaidi mchezo, huku Yanga wakicheza kwa kujihami zaidi.
    Dakika ya tano Godfrey Wambura alimpa krosi nzuri Juma Mahadhi, lakini mshambuliaji huyo alipiga shuti pembeni na kuikosesha Coasfal Union bao la mapema. 
    Yanga walijibu shambulio hilo dakika moja baadaye, lakini mpira uliopigwa na Donald Ngoma aliyepokea krosi ya Issoufou Boubakary ilidakwa na kipa wa Coastal Union Juma Fikirini. 
    Ismail Mohamed wa Coastal aliikosesha timu yake bao baada ya kuchelewa kuunganisha krosi ya Adeyum Ahmed na kumpa nafasi kipa ya Yanga Deogratius Munishi 'Dida' kudaka mpira huo uliokuwa unaelekea langoni mwake dakika ya 10. Coastal Union walifanya shambulio lingine katika dakika ya 30 kupitia kwa Ismail Mohamed, ambaye hata hivyo alichelewa kuunganisha krosi ya Miraji Adam na Dida kuruka juu na kuokoa hatari hiyo. 
    Sekunde chache kabla ya mapumziko Deus Kaseke alipiga juu na kuikosesha Yanga bao kufuatia pasi fupi aliyopokea kutoka kwa Haruna Niyonzima. 
    Mchezo huo ulihamia kwenye dakika 30 za nyongeza baada ya kumalizika kwa sare ya 1-1
    Mshambuliaji wa Burundi, Amissi Tambwe aliyempokea Ngoma kipindi cha pili, akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 101 akimalizia pasi ya Malimi Busungu baada ya krosi ya winga Simon Msuva, ambao wote pia walitokea benchi kipindi cha pili kuchukau nafasi za Kevin Yondan na Issoufou Boubacar.
    Baada ya bao hilo, mchezo ukasimama dakika ya 105 kufuatia mashabiki kuanza kutupa chupa na mawe uwanjani na kumjeruhi mshika kibendera namba mbili, Charles Simon juu ya jicho la kushoto. 
    Refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga akapuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo huo dakika ya 110, huku mashabiki wakiendelea kuushambulia uwanja kwa mawe na chupa.
    Kamisaa wa mechi, Osuri Kosuri kutoka Simiyu alisema kuwa wamelazikika kuvubna mchezo kufuatia vurugu zilizotokea uwanjani. 
    Kosuri alisema kuwa Usalama ulikuwa mdogo uwanjani hapo na askari walishindwa kujimili vurugu. 
    Kuhusu hatima ya mchezo huo, alisema watawasilisha ripoti yao kwa wahusika (TFF) ambao ndiyo wataamua.
    Kuna uwezekano Yanga ikasonga mbele Fainali, kwa sababu Coastal walikuwa nyumbani na wanaweza kubeba msalaba wa mashabiki kufanya vurugu.
    Kikosi cha Coastal Union kilikuwa: Fikirini Bakari, Hamad Juma, Adeyum Ahmed, Hamisi Mbwana, Miraj Adam, Abdulhalim Hamoud, Juma Mahadhi, Yousoufa Sabo, Ismail Mohamed/Ally Ahmed ‘Shiboli’ dk 80, Godfrey Wambura na Ayoub Yahaya. 
    Yanga SC: Deogratius Munishi 'Dida', Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro' Vicent Bossou, Kelvin Yondani/Malimi Busungu dk75, Deus Kaseke, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma/Amissi Tambwe dk81, Haruna Niyonzima na Issoufou/Simon Msuva dk46.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VURUGU ZAVUNJA MECHI YA COASTAL NA YANGA, REFA AJERUHIWA KWA MAWE MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top