• HABARI MPYA

    Saturday, April 30, 2016

    KIVUMBI LIGI KUU LEO, DERBY MBILI...GAME LA KIDUGU MOJA

    Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
    MBIO za kusaka ubingwa na nafasi ya kubaki kwenye Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu ujao zinatarajia kuendelea leo katika viwanja vitano tofauti hapa nchini huku Toto Africans ikiwakaribisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza.
    Mechi ya leo ugenini ya Yanga ni kati ya michezo yake mitano ya ligi iliyobakia itakayofanyika mikoani na itashuka uwanja ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 4-1 iliyopata kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Oktoba 21 mwaka jana.
    Akizungumza Jana kwa simu kutoka jijini Mwanza, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema kuwa wachezaji wake wako tayari na mchezo huo na haamini kwenye ligi kuna timu ambayo ina 'undugu' na Yanga na kutegemea kupata pointi bila kutoa 'jasho'.
    Mabingwa watetezi, Yanga SC wapo Mwanza leo

    Pluijm alisema Yanga itashuka uwanjani ikiwa na lengo moja la kusaka pointi tatu na kutokana na kuifahamu Toto Africans, anajua namna ambayo wataikabili na hatimaye kutimiza lengo la kushinda mchezo huo wa ligi.
    Hata hivyo kocha huyo Mdachi alisema kwamba watacheza kwa tahadhari mchezo huo kwa sababu Jumamosi ijayo wataikaribisha Sagrada Esperanca kutoka Angola katika mechi ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho na wanahitaji kupata ushindi wakiwa nyumbani.
    "Kama tulivyopambana katika mechi nyingine, na kesho (leo) tutafanya hivyo hivyo ili kupata matokeo mazuri, siamini 'undugu' na timu yoyote kwenye ligi au mashindano mengine, jezi ndio zinafanana na si Yanga tu, kuna timu nyingi zinafaa rangi nyekundu na bluu na wanapokutana mpira huchezwa na yenye kiwango cha juu hupata ushindi," Pluijm alisema.
    John Tegete, kocha mkuu wa Toto Africans aliliambia gazeti hili kwamba wakazi wa Kanda ya Ziwa wajitokeze kushuhudia soka la kiwango cha juu na bado timu yake inahitaji kujiweka katika mazingira ya kubaki Ligi Kuu.
    "Hatupendi kupoteza mchezo, tutateremka uwanjani kusaka ushindi, naamini vijana wangu wakiwa makini, Yanga watalala kama walivyolala Simba, siku hizi wamebaki 'majina' na si timu kubwa," Tegete aliongeza.
    Mwadui FC wana shughuli na Stans United leo Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga

    SHINYANGA, TANGA 'DERBY'
    Mchezo mwingine ambao utasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka ni kati ya wapinzani wa mkoa wa Shinyanga Mwadui FC wanaowatarajia kuwakaribisha Stand United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.
    Kocha Mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelu 'Julio' leo atawakaribisha wageni hao kutoka Shinyanga mjini wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliofanyika Desemba 12 kwenye Uwanja wa CCM, Kambarage.
    African Sports wana kazi na Coastal Union leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga leo

    TANGA DERBY MKWAKWANI
    Leo pia timu nyingine za jiji la Tanga Africans Sports itateremka kwenye  Uwanja wa Mkwakwani kuikaribisha Coastal Union huku zote zikiwa katika 'janga' la kushuka daraja.
    Desemba 13 katika mechi ya mzunguko wa kwanza timu zilitoka sare ya bao 1-1 na leo zitakutana huku Coastal Union yenye pointi 22 ikiburuza mkia kwenye msimamo wa ligi wakifuatiwa na African Sports ambao wana pointi 23 na kila moja imecheza mechi 27.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIVUMBI LIGI KUU LEO, DERBY MBILI...GAME LA KIDUGU MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top