• HABARI MPYA

    Friday, April 29, 2016

    MWINYI MNGWALI YUKO FITI 100% KUIVAA TOTO KESHO

    Na Prince Akbar, MWANZA
    BEKI wa kushoto wa Yanga, Mwinyi Hajji Mngwali anatarajiwa kurejea uwanjani kesho timu yake ikimenyana na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Mwinyi amefanya mazoezi vizuri jana kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ameridhishwa na maendeleo yake kwa sasa.
    Beki huyo wa Kizanzibari aliye katika msimu wake wa kwanza Jangwani baada ya kusajiliwa Agosti mwaka jana kutoka KMKM ya Zanzibar, amekosa mechi nne zilizopita kutokana na kuwa majeruhi.
    Mwinyi Hajji Mngwali amepona ana anatarajiwa kurejea uwanjani kesho, Yanga ikimenyana na Toto Mwanza

    Mngwali aliumia katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam timu hizo zikitoka sare ya 1-1.
    Baada ya hapo akakosa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, mchezo wa marudiano na Ahly nchini Misri, Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Coastal Union mjini Tanga na mchezo wa ligi tena dhidi ya Mgambo JKT Jumatano Dar es Salaam.
    Katika mchezo na Mgambo Jumatano, Mwinyi alikuwa benchi kwa mara ya kwanza baada ya kuwa jukwaani katika mechi zote zilizotangulia, huku mkongwe Oscar Joshua akirudishwa uwanjani baada ya kusugua benchi kwa muda mrefu.
    Mabingwa watetezi, Yanga wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 62 baada ya kucheza mechi 25, wakifuatiwa na Azam FC wenye pointi 58 za mechi 25 pia, wakati Simba SC ni ya tatu kwa pointi zake 57 za mechi 25.
    Kwa ujumla Ligi Kuu itaendelea kesho na mbali na Toto na Yanga, African Sports watamenyana na Coastal Union katika mechi ya mahasimu wa Jiji la Tanga, Uwanja wa Mkwakwani, Mwadui FC watamenyana na Stand United katika mechi ya mahasimu wa Shinyanga Uwanja wa Mwadui Complex, Mtibwa Sugar na Mbeya City Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Prisons watakuwa wenyeji wa JKT Ruvu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja na mtamu zaidi baina ya Simba SC na Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWINYI MNGWALI YUKO FITI 100% KUIVAA TOTO KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top