• HABARI MPYA

    Wednesday, April 20, 2016

    YANGA YAFA KIUME KWA AHLY...SASA SHUGHULI NA ESPERANCE

    Na Prince Akbar, ALEXANDRIA
    YANGA SC imetolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa mabao 2-1 na Al Ahly usiku huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora.
    Al Ahly inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2 baada ya awali kulazimisha sare ya 1-1 Uwanja wa Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
    Aliyewafungisha virago Yanga leo alikuwa ni Abdallah Said aliyefunga bao la pili dakika ya sita ya muda wa nyongeza baada ya kukamilika kwa dakika 90 za kawaida za mchezo akimalizia krosi ya  Walid Soliman kutoka upande wa kushoto.
    Donald Ngoma amefunga bao la Yanga leo Borg El Arab mjini Alexandria

    Al Ahly walitangulia kupata bao katika mchezo wa leo kupitia kwa kiungo Hossam Ghaly aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Ahmed Fathi dakika ya 52.

    Mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Dombo Ngoma akaisawazishia Yanga dakika ya 57 kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia Juma Abdul.
    Kwa matokeo hayo, Yanga itamenyana na moja ya timu zilizofuzu Kombe la Shirikisho kuwania nafasi ya kupangwa kwenye makundi.
    Kwa Yanga, hii ni mara ya pili kufikia hatua hiyo baada ya mwaka 2007. Mwaka huo Yanga ilifungwa 3-0 na Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutoa sare 0-0 Mwanza.
    Katika kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho na ilitolewa na El Merreikh ya Sudan, ikitoa sare ya 0-0 Mwanza na kufungwa 2-0 Khartoum.
    Yanga inaweza kukutana tena na Esperance ambayo imeitoa Azam FC ya Tanzania jana kwa jumla ya mabao 4-2, ikishinda 3-0 jana Tunis baada ya kufungwa 2-1 Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza.
    Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe/Malimi Busungu dk68, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Kevin Yondan dk86.
    Al Ahly; Sherif Ekramy; Ahmed Fathi, Rami Rabia, Ahmed Hegazy, Sabri Rahil; Hossan Ashour, Hossam Ghaly, Hussein El Sayed, Moaem Zakaria/Walid Soliman dk64, Ramadan Sobhy na Amr Gamal/ Malick Evouna dk71.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAFA KIUME KWA AHLY...SASA SHUGHULI NA ESPERANCE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top