• HABARI MPYA

  Monday, April 11, 2016

  ULIPAJI WA MIRAHABA NI KIZUNGUNGU …ELIMU KUBWA INAHITAJIKA

  TANGU ilipotangazwa kuwa sasa nyimbo zinazopigwa kwenye vituo vya radio na televisheni zitaanza kulipiwa (mirahaba), kumekuwa na mgawanyiko mkubwa wa fikra miongo mwa mwasanii na wadau wa muziki.
  Wako wanaosema kuwa sasa ukombozi wa wanamuziki umewadia na wako pia wanaoamini kwamba mfumo huu ni kaburi kwa aina fulani ya wanamuziki.
  Wanaosema mfumo huu ni kaburi, wamekuwa wakiendesha vikao vya aina mbali mbali ili kuhakikisha jambo hili linasitishwa lakini kwa bahati mbaya sana kwao, uamuzi huu wa kulipia mirahaba, ni uamuzi uliopitishwa kwa baraka zote za serekali na kwa taratibu zote za kisheria, suala la kusitisha ni sawa na njozi za mchana.

  Mfumo huu umeanza kutumika mwezi Januari mwaka huu na tayari vituo vya radio na televisheni vimeshapelekewa hati ya madai (invoice) kutoka  chama cha hatimiliki - COSOTA kwaajili ya nyimbo zilizopigwa miezi mitatu iliyopita.
  Ingawa jambo hili ni geni hapa Tanzania, lakini inawezekana tumechelewa sana kwani nchi nyingi duniani zimekuwa zikitumia mfumo huu na kuwanufaisha wasanii wengi -Mfumo huu unakuwa ni chanzo kingine cha kumwingizia pesa msanii  nje na utaratibu tuliouzoea wa kutegemea mapato ya viingilio vya mlangoni kwenye kumbi za starehe.
  Lakini pamoja na utamu wote wa jambo hili, bado darasa kubwa linahitajika, vinginevyo utatokea mkanganyiko wa ajabu utakaopelekea mtafaruku mkubwa -Inafika wakati hata wale wanaounga mkono, wengi wao hawajui wanaunga mkono kwa sababu zipi, kwa faida zipi, kwa mgawanyo upi.
  Hali kadhalika wengi miongoni mwa wanaopinga nao hali ni ile ile, hawajui wanapinga kwasababu zipi, sana sana watakuambia ni woga wa nyimbo zao kutopigwa radioni na hivyo kukosa promosheni.
  Kwa bahati mbaya sana ujio wa mfumo huu umeletwa kirahisi kuliko hata ilivyokuwa kuutoa mfumo wa analojia kwenda dijitali …Hakuna elimu kubwa iliyotolewa.
  Wako wasiojua kuwa nyimbo zitalipwa kwa dakika zitakazochezwa, wako watangazaji wanaodhani kuupiga wimbo mmoja kwa kuukatakata na kisha kuingiza porojo za hapa na pale halafu wimbo ukaendelea tena ni kubana matumizi, kumbe wapi.
  Wako wasiojua kuwa kama radio haina matangazo mengi ya biashara basi wimbo wako hata upigwe mara milioni moja hupati lolote. Kwa kifupi nyimbo hizi zinalipwa kutokana na matangazo ya biashara.
  Hivi leo hii bendi kama Msondo Ngoma, Sikinde na FM Academia zilizopita chini ya wamiliki tofauti tofauti zitakuwa na haki ya kumiliki nyimbo zipi? FM hii imiliki nyimbo za FM Musica International?, Msondo hii imiliki nyimbo za Nutta Jazz, Juwana na OTTU Jazz, Sikinde hii imiliki nyimbo za DDC Mlimani Park? Ahhh wapi tusidanganyane, hapa darasa kubwa linahitajika.
  Vipi nyimbo za Chuchu Sound ambayo imeshakufa na mmiliki wake pia ameshafariki, pesa zake zinakwenda wapi, vipi kuhusu nyimbo za Mangwea, Issa Matona Mbaraka Mwishehe na wengine wengi waliotangulia mbele ya haki, pesa zao zinakwenda wapi? Kwa mgawanyo upi?
  Vipi kuhusu tungo za wanamuziki waliojiriwa kwenye mabendi haki zao zikoje? Walioshiriki kutengeneza wimbo wanavuna nini? Maproducer je? Leo ikitokea bendi inasema inataka nyimbo zake zipigwe bure inakuweje? Sheria inaruhusu? Wanamuziki walioshiriki wana haki ya kupinga wazo la mmiliki wao ya kutoa idhini nyimbo kupigwa bure?
  Kampuni ya Copyrights Management East Africa Limited (CMEA) ndiyo iliyoingia mkataba na COSOTA katika kufanya kazi ya kuhakiki nyimbo imepigwa mara ngapi kwenye kituo cha radio na televisheni na unastahili kulipwa shilingi ngapi. Je vituo vya radio na televisheni vitakuwa na uhakika gani kwamba bili waliyoletewa ni sahihi? Je COSOTA inapeleka bili baada ya kujua radio ilikuwa na matangazo mangapi ya biashara au la? Je COSOTA itahakiki vipi bei ya kila tangazo la radio? Haya yote ni maswali ambayo yanahitaji kupata majibu ya kina.
  Binafsi naamini kabla ya mfumo huu haujaanza CMEA, COSOTA, BASATA, Shirikisho la Vyama vya Muziki Tanzania na serikali kwa ujumla wake, zilipaswa kutumia muda mrefu kutoa elimu pana na za gharama kwa njia ya vipindi maalum kwenye televisheni na redioni, makala na matangazo kwenye magazeti na makongomano ya mara kwa mara yatakayoitishwa kwa njia sahihi na sio zile za kiujanja ujanja, lakini pia mwisho wa siku waelewe kuwa muziki hauko Dar es Salaam peke yake na hivyo elimu hii inawahusu pia wa mikoani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ULIPAJI WA MIRAHABA NI KIZUNGUNGU …ELIMU KUBWA INAHITAJIKA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top