• HABARI MPYA

  Thursday, April 07, 2016

  REAL MADRID YAPIGWA 2-0, MAN CITY YALAZIMISHA SARE KWA PSG

  REAL Madrid imepoteza mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufungwa mabao 2-0 usiku wa Jumatano na wenyeji VfL Wolfsburg Uwanja wa Volkswagen Arena.
  Ikitoka kushinda 2-1 dhidi ya mahasimu Barcelona katika La Liga, Real inayofundishwa na Mwanasoka Bora wa zamani wa Dunia, Mfaransa, Zinadine Zidane ilishindwa kufurukuta Ujerumani.
  Mabao ya Wolfsburg yamefungwa na Ricardo Rodriguez kwa penalti dakika ya 18 na Maximilian Arnold dakika ya 25 na sasa Real wanatakiwa kushinda 3-0 nyumbani wiki ijayo ili kwenda Nusu Fainali.
  Wachezaji wa Real Madrid kutoka kushoto, Cristiano Ronaldo, Pepe, Gareth Bale na Karim Benzema wakieanda kinyonge katikati kuanza mpira baada ya kufungwa PICHA ZAIDI GONGA HAPA

  Mchezo mwingine wa Jumatano, Paris Saint-Germain imelazimishwa sare ya 2-2 na Manchester City Uwanja wa 
  Parc des Princes. Mabao ya PSG yamefungwa na Zlatan Ibrahimovic dakika ya 41 na Adrien Rabiot dakika ya 59, wakati ya Man City yamefungwa na Kevin De Bruyne dakika ya 38 na Fernando Luiz Rosa dakika ya 72.
  Beki wa PSG, David Luiz akitelezea mpira miguuni mwa wachezaji wa Man City PICHA ZAIDI GONGA HAPA

  Katika mechi za jana, mabingwa watetezi, Barcelona waliwafunga washiriki wenzao wa La Liga ya Hispania, Atletico Madrid mabao 2-1 Uwanja wa Camp Nou, wakati Bayern Munich ilishinda 1-0 dhidi ya Benfica ya Ureno Uwanja wa Allianz Arena.
  Mshambuliaji wa zamani wa Liverpool na Chelsea za England, Fernando Torres alianza kuifungia  Atletico Madrid dakika ya 25, kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu dakika 10 baadaye kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
  Luis Suarez akaisawazishia Barca dakika ya 63 na kuifungia bao la ushindi dakika ya 74.
  Matokeo hayo, yanamaanisha Barca bado haipo salama, kwani inaweza kutolewa iwapo itafungwa 1-0 katika mchezo wa marudiano mjini Madrid.
  Bao pekee la Arturo Vidal mapema tu dakika ya pili limeipa ushindi wa 1-0 Bayern Munich dhidi ya Benfica. Bayern sasa wana kazi ya ziada ya kwenda kuulinda ushindi wao katika mchezo wa marudiano ugenini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: REAL MADRID YAPIGWA 2-0, MAN CITY YALAZIMISHA SARE KWA PSG Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top