• HABARI MPYA

  Wednesday, April 06, 2016

  NDANDA WAICHOMOLEA AZAM JIONI, COASTAL YAPIGWA TENA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM 
  MATUMAINI ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara yameanza kuyeyuka Azam FC kufuatia kulazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 jioni ya leo na Ndanda FC ya Mtwara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Matokeo hayo yanaifanya Azam FC ijiongezee pointi moja na kufikisha 52 baada ya kucheza mechi 23, wakiwa nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 53 za mechi 22, wakati Simba SC inaongoza kwa pointi zake 57 za mechi 24. 
  Katika mchezo wa leo, Azam FC walikuwa wa kwanza kupata dakika ya 16 kupitia kwa kiungo wake Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyefumua shuti kali baada ya pasi ya kiungo Kipre Balou.
  Wachezaji wa Azam FC na Ndanda FC wakisabahiana kabla ya mchezo leo Uwanja wa Azam Complex

  Mshambuliaji Didier Kavumbagu akaifungia Azam FC bao la pili dakika ya 42 kwa shuti pia akimalizia krosi ya beki Waziri Salum.
  Kipindi cha pili, Ndanda walizinduka na kusawazisha mabao yote – akianza Atupele Green kwa penalti dakika ya 51 baada ya kipa Aishi Manula kuchezea rafu Paul Ngalema ndani ya boksi na refa Ahmad Simba wa Kagera kutenga tuta.
  Zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo kumalizika, Ahmed Msumi alyetokea benchi kipindi cha pili aliifungia Ndanda bao la kusawazisha dakika ya 88 baada ya kufumua shuti la mbali kutokea pembeni.
  Hiyo inakuwa sare ya pili mfululizo kwa Azam FC, baada ya Jumapili kulazimishwa sare ya 1-1 na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Baada ya mchezo huo, Azam FC inarejea kambini kujiandaa na mchezo wake wa kwanza hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia Jumapili mjini Dar es Salaam. 
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, wenyeji Majimaji wameifunga 2-0 Coastal Union Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum/David Mwantika dk46, Aggrey Morris, Racine Diouf/Mudathir Yahya dk46, Serge Wawa, KIpre Bolou, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Didier Kavumbagu/John Bocco dk70, Kipre Tchetche na Ramadhani Singano ‘Messi’. 
  Ndanda FC: Jeremiah Kisubi, Aziz Sibo, Paul Ngalema, Hemed Khoja, Cassian Ponera, William Lucian, Salum Minelly, Masoud Ally/Burhan Rashid dk20, Omary Mponda/Ahmad Msumi dk85, Atupele Green na Kigi Makassy.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDANDA WAICHOMOLEA AZAM JIONI, COASTAL YAPIGWA TENA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top